Jun 10, 2017 03:58 UTC
  • Jumamosi, Juni 10, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 15 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1438 Hijria sawa na tarehe 10 Juni mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Mtukufu Mtume (saw). Imam Hassan (as) alikulia chini ya malezi na usimamizi wa Mtume, Bibi Fatma Zahra binti ya Mtume na Imam Ali (as). Baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ali hapo mwaka wa 40 Hijiria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya Imam huyo. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake Imam, hali iliyomlazimu mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuhifadhi dini tukufu ya Kiislamu. ***

Miaka 227 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 10 Juni 1790 vikosi vya Uingereza viliivamia ardhi ya Malaya inayojulikana hii leo kama Malaysia. Wakati huo Uholanzi ilikuwa ikiikoloni Malaya na kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo wa madini ya bati. Kwa kuingia vikosi vya Uingereza Malaya ilibidi Uholanzi ianze kuondoka nchini humo na ilipofikia mwaka 1824 Uholanzi ilikubali kuiachia Uingereza ardhi hiyo kwa sharti kwamba nayo iachiwe Indonesia ambayo ilikuwa ina umuhimu mkubwa kwa Uholanzi. Malaysia ilijipatia uhuru wake mwaka 1957 na Indonesia mwaka 1956.***

Malaysia

Katika siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, vita vya Marekani na Uingereza vilianza. Miongoni mwa matukio muhimu ya historia ya Marekani katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ni vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili. Sababu ya kuanza vita hivyo inasemekana kuwa ni kuzingirwa Ufaransa na Uingereza kutokea baharini na kuzuiwa safari za meli za Marekani katika maji yanayozunguka nchi za Ulaya. Lakini pamoja na hayo Marekani ilikuwa na sababu zingine za kuanzisha vita hivyo, muhimu kati yazo ikiwa ni madai ya uungaji mkono wa siri wa Uingereza kwa Wahindi Wekundu wa Marekani dhidi ya serikali kuu ya nchi hiyo. Kufuatia vita hivyo, tarehe 18 Juni 1812 askari jeshi wa Marekani walivamia vituo na mali za Uingereza huko Canada na kuuteketeza mji wa Toronto. Vita hivyo vilipamba moto kiasi kwamba, mwezi Agosti 1814 Uingereza ilituma askari wake katika pwani ya mashariki ya Marekani na kuendesha vita hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington DC. Hatimaye mazungumzo ya amani baina ya nchi mbili hizo yalitiwa saini huko Ubelgiji na kupelekea kusimamishwa vita hivyo mwezi Disemba mwaka huhuo wa 1814.  ***

Marekani na Uingereza

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Bani Sadr Rais wa kwanza wa Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliuzuliwa na Imam Khomeini wadhifa wa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote kutokana khiyana na usaliti. Tangu awali baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, Bani Sadr alikumbwa na kiburi na ghururi sana na akawa anafuatilia suala la kuviweka kando vikosi vya mapinduzi vilivyokuwa vitiifu kwa Imam Khomeini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha Bani Sadr alikuwa akishirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu. Bani Sadr alikwamisha utendaji wa serikali kutokana na kukwepa kwake kumkubali Waziri Mkuu Muhammad Rajai mmoja wa wanamapambano mashuhuri aliyekuwa amechaguliwa na Bunge kwa wingi wa kura. Ukwamishaji huo wa Bani Sard ulifikia kilele katika vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran na kupelekea miji mingi ya Iran katika kipindi hicho cha vita kukaliwa kwa mabavu na utawala wa dikteta Saddam Hussein. Hatimaye katika siku kama ya leo, Imam Khomeini alimuuzulu Bani Sadr cheo cha Amiri Jeshi Mkuu. Siku chache baadaye Bunge lilipasisha kwa wingi wa kura mpango kutokuwa na imani na uwezo wa kisiasa Rais huyo.***

Bani Sadr

Na miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo Hafez al-Assad rais wa wakati huo wa Syria aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alizaliwa mwaka 1930. Aliteuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha Syria mwaka 1964 na kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo miaka mitatu baadaye. Hafez al-Assad aliipindua serikali ya wakati huo ya Syria mwaka 1970 na kuchukua uongozi wa nchi hiyo na kisha kuteuliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Asad aliimarisha jeshi la nchi hiyo kiasi kwamba mwaka 1973 alifanikiwa kurejesha sehemu ya milima ya Golan iliyotekwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel katika vita vya 1967. Siasa muhimu za Hafez al-Assad zilikuwa ni za kutofanya mapatano na utawala huo ghasibu. ***

Hafez al-Assad