Jun 16, 2017 23:06 UTC
  • Jumamosi, Juni 17, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 22 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1438 Hijria mwafaka na tarehe 17 Juni 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1165 iliyopita yaani tarehe 22 Ramadhani 273 Hijria, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Ibn Majah alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni. ***

Miaka152 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Haj Abdul-Hussein Tehran aliyekuwa mashuhuri wa jina la Sheikh al-Iraqiyiin. Alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa Iran. Abdul Hussein Tehran alikuwa mwanazoni mkubwa, fakihi na mcha Mungu aliyekuwa na Zuhdi. Aidha alimu huyo alisifika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo. Abdul Hussein Tehran alibobea katika elimu mbalimbali na alikuwa mwalimu asiye na mithili katika masomo ya Fikihi, hadithi na Tasiri ya Qur'ani. Aidha msomi huyo alikuwa na mapenzi ya kukusanyua vitabu vya madhehebu mbalimbali. Aliitoa wakfu maktaba yake kubwa na tajiri kwa vitabu kwa ajili ya watafiti na watu wa kufanya mutwalaa.***

Haj Abdul-Hussein Tehran

Katika siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku dunia. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran. ***

Shirika la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali

Na miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 27 Khordad 1358 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuanzishwa Jihadi ya Ujenzi wa taifa kwa lengo la kujitawala na kujitosheleza taifa la Iran na kujikwamua na umasikini na matatizo mbalimbali hasa vijijini. Kufuatia amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wanachuo na vijana wenye imani na wasomi waliungana ili kujenga na kukarabati maeneo yaliyokuwa duni na yaliyokuwa nyuma kimaendeleo. Jihadi ya ujenzi wa taifa ambayo ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ilibadilisha sura ya maeneo mbalimbali duni nchini, kutokana na hatua muhimu zilizochukuliwa za ujenzi wa miundo mbinu. Baadaye jihadi ya ujenzi ilibadilishwa na kuwa wizara na kisha kuunganishwa na wizara ya kilimo na kuwa Wizara ya Jihadi ya Kilimo. ***