Jun 18, 2017 03:56 UTC
  •  Jumapili, Juni 18, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 23 Ramadhani 1438 Hijria sawa na tarehe 18 Juni,  2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 220 iliyopita, alifariki dunia kwa kuuawa huko Georgia, Agha Mohammad Khan Qajar, mfalme wa kwanza wa utawala wa Qajar nchini Iran. Agha Mohammad Khan Qajar alikuwa mtawala muovu sana nchini hapa. Baada ya kuangamizwa silsila ya watawala wa Zand, Khan Qajar aliingia madarakani kupitia udanganyifu, ukatili, umwagaji damu mkubwa na jinai zisizo na mfano dhidi ya Wairani huku mwaka 1174 Hijiria Shamsia akivishwa taji la kifalme mjini Tehran na hivyo akawa ameasisi utawala wa kiimla nchini. Katika kipindi cha utawala wake, maeneo tofauti ya Iran yalitangaza kujitenga kutokana na mtawala huyo kukosa weledi wa uongozi, kuendeleza anasa na kutenda jinai nyingi. Hata hivyo miaka miwili baadaye akiongoza jeshi la Iran kuishambulia Caucasus na Georgia, Agha Mohammad Khan Qajar aliuawa na wafanyakazi wake wawili na hivyo maisha yake yenye faili jeusi yakafikia tamati akiwa na umri wa miaka 63.

Agha Mohammad Khan Qajar,

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, vilianza vita vya kihistoria vya Waterloo, vita vya mwisho vya Napoleon Banaparte na madola ya Ulaya. Katika vita hivyo majeshi ya serikali za Prussia na Uingereza yalikutana uso kwa uso na majeshi ya Napoleon Banaparte katika eneo lililokuwa likiitwa kwa jina la Waterloo. Katika vita hivyo na kutokana na kunyesha mvua kali na kuharibika njia zilizokuwa zikitumiwa kwa usafirishaji, hivyo zana za kijeshi  zilichelewa kufika uwanja wa vita sambamba na kuchelewa kufika kikosi cha mstari wa mbele cha Wafaransa. Kufuatia hali hiyo, Napoleon Banaparte akawa ameshindwa vibaya katika vita hiyo na hivyo kumfanya akimbie kwa kutumia meli kuelekea kisiwa cha Saint Helena na kufariki dunia miaka kadhaa baadaye kwenye kisiwa hicho.

Vita vya kihistoria vya Waterloo

Siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu. Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta zinazopatikana katika kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 huku akitumia karibu muda wa miaka 30 katika uandishi wake na kutokea kuitwa kwa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Katika kipindi cha maisha yake kulitawala hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu.

Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, Maxim Gorky, fasihi na mwandishi mashuhuri wa nchini Russia. Alexei Maximovich Peshkov maarufu kwa jna la Gorky, alikuwa mandishi mkubwa aliyezaliwa tarehe 28 Machi 1868 Miladia katika mji wa Gorky nchini Russia. Alianza kusoma kwa bidii elimu ya fasihi hapo mwaka 1895 na kupewa lakabu ya Maxim Gorky ambayo ilikuja kutumika kama jina lake na baadaye kufikia kupata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kwa kuzingatia kuwa alitokana na familia masikini, hivyo uandishi wa Maxim Gorky ulijikita sana katika kupiga vita umasikini na ujinga. Ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu cha Mijeledi Mitatu kinachozungumzia maisha yake.

Maxim Gorky

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita inayosadifiana na tarehe 18 Juni 1953 nchi ya Misri ilitangazwa kuwa ya Jamhuri na Mfalme Farouq wa Misri na wanawe wakabaidishwa. Kufuatia kushindwa Misri katika vita na Israel mwaka 1948, wananchi wa Misri walipoteza imani yao kwa Mfalme Farouq na hivyo hali ya ndani ya nchi hiyo ikaanza kuharibika. Mwishowe liliundwa shirika la siri ndani ya jeshi lililopinga utawala wa mfalme huyo. Mwaka 1952 shirika hilo lilimlazimisha Mfalme Farouq kujiuzulu kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Muhammad Najib na Jamal Abdun Nassir. Mwaka mmoja baada ya kutangazwa Jamhuri ya Misri, Jenerali Muhammad Najib aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Misri. Mwaka mmoja baadaye Jamal Abdul Nassir alimuuzulu Muhammad Najib. Abdul Nassir alipata umaarufu mkubwa nchini Misri na duniani kote kwa sababu ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mfalme Farouq wa Misri

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini sana za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano ya pili ya kupunguza silaha yaliyojulikana kwa jina la Salt 2 kati ya Marais Leonid Brezhnev wa Urusi ya zamani na Jimmy Carter wa Marekani. Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kupunguza silaha za nyuklia duniani.

Utilianaji saini wa mkataba wa Salt 2

Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, Najimudin Erbakan Waziri Mkuu aliyekuwa na misimamo ya Kiislamu wa Uturuki alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya wanajeshi wa nchi hiyo. Chama cha Erbakan kilipata kura nyingi katika uchaguzi wa Disemba mwaka 1994 na kuunda Baraza la Mawaziri. Lakini wasekulari na makamanda wa jeshi walizuia kutekelezwa malengo ya serikali yake. Waziri Mkuu huyo alikuwa akiamini kwamba kuwakandamiza wanaharaki wa Kiislamu nchini Uturuki ni kinyume na demokrasia na alipinga kuimarishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel. Lakini Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa wa wanajeshi Februari 1997 lilitoa amri ya kumlazimisha Erbakan akabiliane na wanaharakati wa Kiislamu. Miezi minne baadaye waziri mkuu huyo alishtakiwa mahakamani kutokana na misimamo yake ya Kiislamu na kuzuiwa kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa muda wa miaka mitano.

Najimudin Erbakan