Jun 19, 2017 16:12 UTC
  • Jumatatu tarehe 19 Juni, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Ramadhani 1438 Hijria, sawa na tarehe 19 Juni, 2017.

Siku kama ya leo miaka 728 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.

Qutbuddin Shirazi

Tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1877, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri. Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu wa Kipolandi, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake.

Enrico Forlanini

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.

Bendera ya Kuwait

Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, sawa na tarehe 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati mwandishi na msomi wa zama hizi wa Kiirani mjini London, Uingereza. Dakta Shariati alipata elimu yake ya juu katika taaluma ya fasihi sambamba na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa mfalme hapa nchini. Dakta Shariati alikuwa bega kwa bega na Shahidi Mutahhari na Shahidi Bahonar, katika kuanzisha Husseiniya ya Ershad mjini Tehran kwa shabaha ya kuzikomaza fikra za tabaka la vijana. Ameandika zaidi ya vitabu 200 na miongoni mwao ni 'Uislamu na Mwanadamu', 'Historia ya Ustaarabu' na 'Fatima ni Fatima'.

Dakta Ali Shariati

 

Tags