Alkhamisi 22 Juni, 2017
Leo ni Alkhamisi 27 Ramadhani 1438 Hijria inayosadifiana na Juni 22, 2017.
Miaka 36 iliyopita sawa na tarehe Mosi Tir mwaka 1360 kwa mujibu wa Kalenda ya Kiirani, hayati Imam Ruhullah Khomeini alipasisha uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu wa kutokuwa na imani na rais wa wakati huo Abul Hassan Bani Sadr na kwa utaratibu huo kiongozi huyo akalazimika kung'atuka madarakani. Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda. Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, katika Vita vya Pili vya Dunia, jeshi la Ujerumani ya Kinazi lilianza mashambulizi makubwa dhidi ya Urusi ya zamani kwa jina la Operesheni ya Barbarossa. Kwa utaratibu huo Adolph Hitler akaanzisha vita vingine katika upande wa mashariki mwa Ujerumani kwa shabaha ya kutimiza mipango yake ya kutaka kujitanua zaidi. Hadi wakati huo tayari dikteta huyo alikuwa ameteka nchi kadhaa za Ulaya.
Katika operesheni hizo, askari wa Ujerumani walisonga mbele na kufika katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Moscow. Hata hivyo jeshi la Ujerumani lilipata matatizo makubwa kufuatia kuanza kipindi cha baridi kali na hivyo likashindwa kusonga mbele. Wananchi na jeshi la Urusi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan Moscow, Leningrad na Stalingrad walipambana vikali na jeshi hilo vamizi na kulilazimisha kurudi nyuma. Mwezi Agosti 1944 jeshi la Urusi lilifika katika mipaka ya Ujerumani.
Miaka 384 iliyopita katika siku kama hii ya leo mnajimu, mtaalamu wa hisabati na mwanafizikia wa Italia Galileo Galilei alilazimika kukana itikadi zake za kisayansi na kielimu mbele ya viongozi wa Kanisa. Mwaka 1632 Galilei aliandika kitabu akijibu na kukosoa mitazamo ya Betlemosi kuhusu sayari ya jua na kutangaza kuwa dunia inazunguma jua. Mwaka mmoja baadaye Papa wa Kanisa Katoliki alimwita Galileo mjini Roma na kuitaja mitazamo hiyo ya kisayansi kuwa ukafiri. Kwa msingi huo, kanisa lilimlazimisha Galileo akane itikadi zake za kielimu la sivyo akabiliwe na adhabu ya kifo. Japokuwa msomi huyo alikana mitazamo yake hiyo ya kielimu kidhahiri tu lakini wakati alipotoka nje ya mahakama alipiga chini mguu wake na kuiambia ardhi: "Licha ya haya yote lakini wewe unazunguka."
Siku kama ya leo miaka 328 iliyopita aliaga dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Allamah Majlisi aliandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa sala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Uislamu na Ahlul Bait zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na umashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.
Na miaka 878 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".