Jun 23, 2017 00:07 UTC
  • Ijumaa, 23 Juni, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Ramadhani 1438 Hijria inayosadifiana na 23 Juni, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1097 iliyopita lilindwa bunge la kwanza duniani huko Island. Bunge hilo ambalo wawakilishi wake walikuwa wakichaguliwa na wananchi kupitia masanduku ya kura, lilikuwa na kazi ya kuisaidia serikali kifikra. Bunge la zamani zaidi duniani baada ya lile la Iceland, lilianza kazi zake nchini Uingereza katikati ya karne ya 13.

Siku lama ya leo miaka 481 iliyopita, ilianza harakati ya kiongozi wa kidini na mpenda mageuzi wa Ufaransa Calvin John huko Geneva mji mkuu wa Uswisi. Alizaliwa mwaka 1509 Miladia na kujifunza sheria na masomo ya kidini. Katika zama za ujana wake, Calvin John alijiunga na harakati ya Kiprotestanti ilioasisiwa na Martin Luther. Aliivamia Geneva Uswisi kwa kusaidiwa na wafuasi wa Kiprotestanti na kujaribu kuasisi mfumo wa uongozi wa kidini katika jamii ya nchi hiyo kwa mujibu wa dhehebu la Protestanti. Calvin John pia alianzisha mfumo wa ideolojia ya Kikristo iliyojulikana kama Calvinism na kubainisha itikadi zake katika kitabu chake alichokiita" Institutes of Christian Religion."

Calvin John

Miaka 260 iliyopita na katika siku mwafaka na leo, vilijiri vita vya kwanza kati ya vikosi vya Uingereza na India huko katika eneo la Bengali kaskazini mashariki mwa India. Waingereza walishinda vita hivyo na kulidhibiti eneo hilo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya India. Waingereza ambao walianza kuingia nchini India miaka kadhaa nyuma kupitia East Indian Company, mbali na kuyarejesha nyuma majeshi ya India, katika vita vilivyofuata ilimshinda pia hasimu wake mkubwa Ufaransa na kufanikiwa kuyatoa kabisa majeshi hayo katika ardhi ya India.

Tarehe 23 Juni miaka 78 iliyopita, Wafaransa waliikabidhi Uturuki bandari muhimu ya Iskenderun, eneo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya Syria. Kwa miaka kadhaa kabla ya tukio hilo, Uturuki ilikuwa ikidai umiliki wa bandari hiyo. Hata hivyo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, eneo hilo lilikabidhiwa Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa baina ya Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo baada ya kuangushwa utawala wa Othmania na kuchukua hatamu za uongozi nchini Uturuki, Mustafa Kamal Ataturk aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi Ufaransa ambayo wakati huo ilikuwa ikiikalia kwa mabavu Syria, iliikabidhi Bandari ya Iskenderun kwa Uturuki. Hatua hiyo ilipelekea kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Ufaransa nchini Syria na kusababisha mapambano dhidi ya mkoloni huyo kuongezeka. Hadi leo hii serikali ya Syria ingali inasisitiza kwamba, Bandari ya Iskenderun ni mali yake.

Bandari ya Iskenderun

Na siku kama ya leo miaka 1166 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri kabisa wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah.