Jul 03, 2017 23:17 UTC
  • Jumanne 4 Julai, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 9 Shawwal, mwaka 1438 Hijiria, sawa na tarehe 4 Julai 2017.

Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Allama Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Hauza ya Kiislamu ya mji wa Najaf akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa na alikuwa mashairi pia. Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua. Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."

Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Marekani. Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino yaani mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu.

Bendera ya Ufilipino

Miaka 241 iliyopita, wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Tangazo la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 Miladia wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la Marekani. Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani.

Bendera ya Marekani

Siku kama ya leo miaka 1328 iliyopita katika siku kama ya leo, Ibn Sirin mpokezi wa hadithi na faqihi mashuhuri wa karne ya pili Hijria aliaga dunia. Ibn Sirin alizaliwa katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Msomi huyo wa Kiislamu alitoa umuhimu mkubwa kwa hadithi za Mtume Muhammad SAW na alikuwa mahiri katika kuhifadhi na kunukuu hadithi. Alikutana na masahaba 30 wa Mtume Muhammad (saw). Ibn Sirin ameacha vitabu na makala nyingi zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali.