Alkhamisi Julai 6, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Shawwal 1438 Hijria, sawa na 06 Julai 2017.
Tarehe 11 Shawwal miaka 1441 iliyopita Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Twaif karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami yake na mlezi wake kipenzi Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraishi wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Twaif wangekubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume mtukufu.
Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na alivutiwa sana na somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni hizo zingali zinatumiwa hadi leo hii.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika vitabu vya riwaya mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson, mwandishi mwenzake wa Kimarekani. Katika riwaya zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya iliyokuwa ikitawala jamii ya Marekani hususan ubaguzi wa kimbari dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika uandishi wa sawa wa riwaya nchini Marekani. Miongoni mwa riwaya za mwandishi huyo ni The Sound and the Fury (1929), As I Lay Dying (1930), Light in August (1932), na Absalom, Absalom! (1936).
Tarehe 6 Julai miaka 53 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Malawi ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na Tanzania, Zambia na Msumbiji.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo baada ya wafanyabiashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia. Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 huku ikipatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi.
Na tarehe 15 Tir miaka 31 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Jawad Khamenei, baba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei. Sayyid Jawad alizaliwa mwaka 1313 Hijia katika mji wa Khamene karibu na Tabriz katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki. Alifanya safari za mara kwa mara katika maeneo matakatifu ya Iraq na Masha'had ambazo zilimtunuku hali ya usafi wa kiroho na kimaanani. Safari hizo zilikuwa na taathira kubwa katika nafsi yake na akaamua kuishi katika mji mtakatifu wa Mash'had ambako alipata elimu kwa maulaa makubwa wa zama hizo. Mwaka 1305 Sayyid Jawad Khamenei alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu na kusoma kwa walimu mashuhuri kama Allamah Mirza Naini na Sayyid Abul Hassan Isfahani. Baada ya miaka mingi ya kufundisha na kulea maulamaa wa baadaye, msomi huyo aliyeishi maisha ya kimaskini, uchamungu na zuhudi kubwa aliaga dunia katika siku kama hii ya leo akiwa na umri wa miaka 91. Amezikwa katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Ali bin Mussa al Ridhaa mjini Mash'had.