Jul 07, 2017 22:19 UTC
  • Jumamosi, Julai 8, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 13 mfunguo Mosi Shawwal 1438 Hijria mwafaka na tarehe 8 Julai mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 527 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Zeinudin bin Ali Shami maarufu kwa jina la Shahidi Thani, mwandishi wa kitabu cha Sherh Lum'a. Alikuwa fakihi na mwanazuoni mahiri wa Kishia. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali kwa baba yake, Shahidi Thani alijiendeleza kielimu kwa wanazuoni wengine wa zama hizo na kuondokea kuwa mmoja wa wasomi watajika wa Kishia. Aidha alifanya safari katika maeneo mbalimbali ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kufanya uhakiki. Alifanikiwa pia kulea wanafunzi wengi waliondokea kuwa wasomi mahiri. Kufuatia njama zilizofanywa dhidi yake Zeinudin alitiwa mbaroni na mwaka 966  Hijria akauawa shahidi. ***

Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, Ayatullah Sheikh Muhammad Twaha, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 83. Familia ya msomi huyo mkubwa inatokana na moja ya familia za maulama mashuhuri wa Kiislamu. Sheikh Twaha alizaliwa na mjini Najaf, Iraq huku akiwa mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Murtadha Answari, alim na faqihi mkubwa katika zama hizo. Aidha Aidha sheikh Twaha alitabahari katika elimu ya fiq’hi, usulu fiq’hi, hadithi na tafsiri ya Qur’ani Tukufu.***

Sheikh Muhammad Twaha

Miaka 100 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Mirza Muhamamad Taqi Shirazi Kiongozi wa Mapinduzi ya Iraq alitoa fatuwa ya jihadi dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya Uingereza kutangaza vita dhidi ya utawala wa Othmania mwaka 1914 na kukaliwa kwa mabavu mji wa Basra, maulamaa wakubwa wa Najaf walitoa hukumu ya kukabiliana na mkoloni huyo. Miaka ya baadaye ilishuhudia kujitokeza makundi yaliyokuwa yakipinga uwepo wa Uingereza nchini Iraq. ***

Mirza Muhammad Taqi Shirazi

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Borujerdi Marjaa Taqlidi aliaga dunia. Alimu huyo mkubwa wa Kishia alizaliwa katika mji wa Borujerd nchini Iran. Sayyid Hussein Tabatabai Borujerdi alikuwa amebobea katika elimu ya hadithi. Kipindi fulani alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na kubakia mjini humo kwa miaka minane. Alikuwa na wanafunzi wengi ambao baadaye walikuja kufahamika kuwa wanazuoni mahiri. Miongoni mwa wanafunzi hao ni Sayyid Muhammad Hussein Beheshti, Ayatullah Jaafar Sobhani, Ayatullah Fazel Lankarani, Ayatullah Nasser Makarem Shirazi na wengine wengi. ***

Sayyid Hussein Borujerdi

Na miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha Uwaziri Mkuu. Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.

Kim Il-sung