Jul 19, 2017 21:52 UTC
  • Alkhamisi 20 Julai, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Shawwal 1438 Hijria sawa na Julai 20, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1290 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18 Miladia, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon ya kuikalia kwa mabavu Uhispania ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi.

Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia kufuatia kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati.

Georg Friedrich Bernhard Riemann

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana  mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya.

Guglielmo Marconi

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo.

Bendera ya Cyprus

Na siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda.

Neil Armstrong