Jul 22, 2017 22:17 UTC
  • Jumapili Julai 23, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 28 Shawwal mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 23 Julai, 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 965 iliyopita na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, alizaliwa Mujaddidu Ibn Adam, maarufu kwa jina la Sinai Ghazni, mtaalamu wa elimu ya Irfan na malenga mkubwa wa Iran katika mji wa Ghaznain, moja ya miji ya Iran ya kale na  moja ya miji ya katikati mwa Afghanistan ya leo. Akiwa kijana alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala ambapo hata hivyo hakudumu sana katika kazi hiyo na kuamua kuachana nayo na kusomea elimu ya Irfan. Baada ya kutabahari katika elimu hiyo, Mujaddidu Ibn Adam alianza kuwatumikia raia sambamba na kuwakosoa watawala dhalimu na wakatili. Moja ya athari muhimu za msomi huyo ni pamoja na kitabu alichokipa jina la 'Hadiqatul-Haqiiqat' na 'Twariiqatul-al-Tahqiq.'

Sinai Ghazni

Siku kama ya leo miaka 254 iliyopita alifariki dunia mwanafasihi na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa Pierre Marivaux. Marivaux  alizaliwa tarehe 17 Novemba mwaka 1688 Miladia mjini Paris, Ufaransa. Mwanafasihi huyu alianza kujishughulisha na sanaa akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kufahamiana na wanafikra na wataalamu wa fasihi wa nchi hiyo na alifanya kazi hiyo ya kuigiza kwa miaka kadhaa katika majumba ya mchezo huo hadi alipoanza kuandika michezo hiyo mwenyewe. Pierre Marivaux alipata umashuhuri mkubwa haraka kutokana na kipawa chake kikubwa cha ukosoaji na uwezo wake mkubwa wa uandishi wa fasihi. Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo ni mchezo wa kuigiza wa The Prudent and Equitable Father, The Triumpth of Love, The Life of Marianne na The Fortunate Peasant.

Pierre Marivaux

Siku kama hii ya leo miaka 219 iliyopita jeshi la Napoleon liliwasili katika mji wa Cairo na mji huo ukakaliwa kijeshi na wavamizi wa Kifaransa. Utawala wa silsila ya Mamaliki ulifikia kikomo huko Misri baada ya mji wa Cairo kukaliwa kwa mabavu na wavamizi wa Kifaransa. Napoleon alielekea Cairo mji mkubwa zaidi wa Misri ambao pia ulikuwa mji mkuu wa utawala wa silsila ya Mamalik baada ya jeshi lake kuikalia kwa mabavu bandari ya Alexandria kwa kutumia zana za kisasa za kivita.

Napoleon

Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita kulivumbuliwa kwa mara ya kwanza mashine ya uandishi (typewriter). Tarehe 23 Julai mwaka 1829 Miladia William Barrett raia wa Marekani aliweka rekodi kufuatia kuvumbua na kutengeza mashine hiyo ya uandishi katika jimbo la Michigan nchini humo. Hata hivyo baada ya hapo hakukuwa na harakati zozote za kuendeleza mashine hiyo. Miaka 31 baadaye yaani sawa na mwaka 1867 Miladia, vijana watatu wa Marekani kwa majina ya Christopher Scholl, Carlos Glydn na Samuwel, walifanikiwa kutengeneza mashine ya kuandikia katika mji wa Milwaukee jimbo la Wisconsin nchini humo, mashine ambayo utumiaji wake ulikuwa mwepesi na rahisi. Hata hivyo ni vyema kuashiria kuwa, juhudi za kuunda mashine ya uandishi zilianza tangu karne ya 14 Miladia, lakini zikaja kuzaa matunda kuanzia karne ya 18 Miladia.

Mashine ya Uandishi

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita, alizaliwa Ernst Herzfeld mtaalamu wa Ujerumani wa masuala ya mashariki ya dunia na Iran. Alikuwa na umahiri mkubwa katika kufahamu ada na lugha za watu wa zamani. Herzfeld alifahamu vizuri historia ya kale ya Iran na Iraq ambapo pia alifundisha kwa miaka mingi katika chuo kikuu cha Berlin, Ujerumani historia hiyo. Aidha alipata kuandika yapata vitabu na makala mbalimbali 190 kuhusiana na historia ya lugha ya Kifarsi na dini tukufu ya Uislamu. Kitabu cha 'Iran na Mashariki ya Zamani' ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Ernst Herzfeld alifariki dunia mwaka 1947.

Ernst Herzfeld

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, alifariki dunia Allamah Sayyid Hüseyn Badkubeyi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu na falsafa. Badkubeyi alizaliwa mwaka 1293 Hijiria karibu na mji wa Baku ambao ni mji mkuu wa Azerbaijan ya leo. Alianza kusoma masomo ya msingi ya dini ya Kiislamu kutoka kwa baba yake. Baada ya kufariki dunia baba yake msomi huyo mkubwa  alielekea mjini Tehran na kusomea elimu ya fiqhi, usulu fiqhi na falsafa kwa muda wa miaka saba kutoka kwa mauala wakubwa wa zama hizo. Kisha alielekea mjini Najaf, Iraq na kuendelea kusoma elimu mbalimbali za Kiislamu kutoka kwa wasomi wa mji huo. Baadaye alianza kufundisha mjini hapo kwa muda wa miaka 14 hususan elimu ya falsafa na kuweza kulea wanafunzi wengi katika uwanja huo. Alikuwa maarufu kwa uchaji-Mungu na zuhdi ya hali ya juu.

Allamah Sayyid Hüseyn Badkubeyi,

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita kulijiri mapiduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Sir Dawda Jawara wa Gambia. Gambia ilianza kujitangazia mamlaka ya ndani mwaka 1962 kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Mwaka 1965 na baada ya kujitangazia uhuru ilijiunga na Umoja wa Mataifa ambapo mwaka 1966 Dawda Jawara alitangazwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Mwaka 1981 wakati Jawara alipokuwa mjini London kulifanyika mapinduzi ya kijeshi ambayo hata hivyo yalisambaratishwa kwa uingiliaji wa kijeshi wa askari wa Senegal ambapo hatimaye Jawara aliweza kurejea tena madarakani. Tarehe 23 Julai mwaka 1994 Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh aliongoza tena mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Jawara na kumlazimu kiongozi huyo akimbie nchi. Mwaka 1984 Dawda Jawara aliongoza tume ya upatanishi iliyochaguliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kati ya Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Dawda Jawara, rais wa zamani wa Gambia