Jul 24, 2017 06:39 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Julai 24

Ufuatao ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Riadha: Iran yazoa medali chungu nzima London

Wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kochokocho katika mashindano ya kimataifa ya wanariadha bingwa wenye ulemavu nchini Uingereza. Hadi tunaenda mitamboni, wanariadha wa Iran ya Kiislamu walikuwa wameshinda medali 20, zikiwemo dhahabu 3 katika michezo mbali mbali. Siku ya Jumamosi, kijana chipukizi Saman Pakbaz mwenye umri wa miaka 22 aliipa Iran medali ya dhahabu katika mchezo wa kurusha kitufe (shot put) umbali wa mita 15.8, mbali na kunyakua medali nyingine ya fedha katika mchezo wa kurusha kisahani (discus), baada ya kukirisha umbali wa mita 50.

Wanariadha wa Iran wameng'ara katika michezo tofauti katika mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kama World Para Athletics Championships mwaka huu 2017; ambapo kwa ujumla wameondoka na medali 3 za dhahabu, 12 za fedha na shaba 5. Duru ya 8 ya mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika katika mji mkuu wa Uingereza, London kwa kuwaleta pamoja wanariadha kutoka nchi mbalimbali, ambayo awali yalifahamika kama International Paralympic Committee (IPC), yalianza Julai 14 na kufunga pazia lake Julai 23.

Oman yazima ndoto ya Iran Kombe la Asia

Ndoto ya timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya kushiriki fainali za michuano ya timu bingwa barani Asia AFC imekatizwa baada ya vijana hao kuchabangwa mabao 2-0 na Oman. Kwa kichapo hicho, vijana wa mkufunzi Amirhossein Peyrovani wametupwa nje ya mechi za kusaka tiketi ya kushiriki mashindano hayo ya kikanda, licha ya kuichachawiza mwenyeji Kyrgyzstan mabao 2-1 katika mchuano wake wa ufunguzi. Iran ilikuwa katika Kundi A pamoja na Oman, Kygyzstan na Sri Lanka ambayo alitangaza kujiondoa kwenye mashindano hayo.

Iran ikivaana na Oman

Nchi 5 kati ya 16 zitakazofuzu katika mechi za kusaka tiketi, zitashiriki mashindano hayo ya AFC Championship Januari mwakani, ikiwemo mwenyeji China ambayo ina tiketi ya moja kwa moja. Hata hivyo timu hiyo imesema itashiriki mechi za muondoano, na iwapo itaambulia nafasi ya 5, basi timu ya 6 itaruhusiwa kushiriki mashindano hayo ya kikanda.

TP Mazembe Hoyee!

Kwa mara nyingine klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeonyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali baada ya kutwaa Ligi Kuu ya Soka nchini humo.  Mazembe iliichachafya klabu ya AS Vita ya Kinshasa bao 1 la uchungu bila jibu katika mchuano wa fainali uliopigwa Jumatano katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi. Bao hilo la pekee na la uishindi la Mazembe lilifungwa na Daniel Adjei raia wa Ghana katika dakika ya pili ya mchuano huo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa mchezaji mwenzake Jo Issama Mpeko. Vijana wa Mazembe ambao walishinda taji hili mwaka uliopita, wamemaliza ligi hiyo ya duru ya 22 kwa alama 33 katika mechi 14 za mwondoano ilizocheza. Hili ni taji la 16 kutwaliwa na klabu hiyo inayomilikiwa na mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.

Mbali na mwaka huu na mwaka jana, TP Mazembe imewahi kushinda taji hili katika ligi za mwaka 1966, 1967, 1969, 1976, 1987, 2000, 2001, 2006, 2007, 2009, 2011, 2012, 2013 na 2014.

Sare tasa dhidi ya Rwanda yaiponza Tanzania

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars iliambulia sare tasa iliposhuka dimbani Jumamosi Jijini Kigali, Rwanda kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) dhidi ya Rwanda, inayofahamika kama Amavubi. Mchezo huo ulikuwa wa marudiano baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Jumaosi iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Vijana wa Stars walihitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 ili wasonge mbele. Sare hiyo imeikosesha vijana wa Stars nafasi ya kuelekea kufuzu kwa mara ya pili kwa fainali hizo baada ya kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2009 nchini Ivory Coast. Kocha wa Taifa Stars anashikilia kuwa, kuvunjika kwa mwiko, sio mwisho wa kusonga sima.

Klabu ya TP Mazembe

Masaibu ya ulimwengu wa soka Tanzania hayakuishia hapo, timu ya soka ya Zanzibar imevuliwa uanachama katika Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) miezi minne baada ya kuidhinishwa. Rais wa CAF Ahmad Ahmad amesema Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haikustahili kukubaliwa kuwa mwanachama wa 55 wa shirikisho hilo mwezi Machi, kwa mujibu wa miongozi na hati za Umoja wa Afrika na Umoja awa Mataifa. Amesema: "CAF haiwezi kukubalia uanachama wa mashirikisho mawili kutoka kwa taifa moja." Shirikisho la Soka Duniani FIFA lilikataa kuipokea Zanzibar kama mwanachama hata baada ya hatua ya CAF, iliyoidhinishwa na mtangulizi wa Ahmad, Issa Hayatou. Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa mwaka 2000, Zanzibar ilipata uanachama wa muda wa CAF, ambapo iliruhusiwa kushirikisha klabu zake katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa.

Raga: Kenya yaidhalilisha Zimbabwe

Timu ya raga ya Kenya maarufu kama Simbas imepata ushindi wake wa tatu mfululizo katika mashindao ya Raga ya Afrika (Africa Gold Cup) baada ya kuidhalilisha Zimbabwe kwa alama 41-22 katika mechi ya kusisimua iliyochezwa Jumamosi uwanjani Hartsfield mjini Bulawayo.

Zimbabwe, ambayo ilipepetwa 61-15 na Kenya mwaka 2016 jijini Harare, ilifunga pointi zake 22 kutoka kwa Hilton Mudariki, Takudzwa Kumadiro na Tichafara Makwanya. Mara ya mwisho Simbas ilikuwa imezuru Bulawayo ilizabwa 24-15 mwaka 2004. Kenya itafunga kampeni yake dhidi ya Namibia hapo Julai 29 jijini Windhoek.

Katika mechi nyingine ya Gold Cup iliyopigwa Jumamosi, mabingwa mara sita wa Afrika, Namibia, walipepeta wenyeji wao Uganda 48-24 jijini Kampala.

Michuano ya kimataifa ya kirafiki

Katika mfululizo wa mechi za kimataifa za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa kwa msimu ujao wa ligi, mechi zilizonoga na zinazozungumziwa sana ni ile kati ya The Blues na The Gunners, na Man U na Madrid. Katika mchuano wa kwanza, klabu ya Uingereza ya Chelsea iliamua kuigeuza Arsenal kichwa cha mwendawazimu na kuinyoa kwa chupa kwa kuisasambua mabao 3-0. Nyota wa mchuano huo alikuwa Mbelgiji Michy Batschuayi ambaye kafunga mabao 2, mbali kuchangia bao la mchezaji mwenza, kiungo William.

Wachezaji wa Madrid wakishangilia goli

Ni chini ya miezi miwili tangu Arsenal iishinde Chelsea mabao 2-1 katika fainali ya kombe la FA uwanjani Wembley. Kwengineko, klabu ya Manchester United walipata ushindi hafifu wa mabao 2-1 kupitia mikwaju ya penati katika mchuano wa kirafiki dhidi ya Real Madrid. Hii ni baada ya timu hizo kukabana koo na dakika 90 za ada kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Katika mchuno huo wa International Champions Cup (ICC), unaofanyika kila mwaka kama sehemu ya timu kujinoa kwa ajili ya msimu mpya wa ligi, Man U walikuwa wa kwanza kucheka na nyavu za Madrid kupitia kiungo Jesse Lingard kunako dakika ya 45.

Hata hivyo kiungo chipukizi mwenye miaka 25 Carlos Henrique Casemiro alisawazisha mambio kupitia mkwaju wa penati kunako dakika ya 68, baada ya kiungo wa Mashetani Wekundu Victor Lindelof kumuangusha Theo Hernandez katika eneo la hatari. Man U ambao wameng'ara katika mechi zote nne za kirafiki, inatazamiwa kuvaan na Barcelona Jumatano hii.

…………………….TAMATI…………………