Jul 25, 2017 03:01 UTC
  • Jumanne tarehe 25 Julai, 2017

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Dhilqaada 1438 Hijria sawa na Julai 25, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1265 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya kutegemewa, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan huko kaskazini mashariki mwa Iran kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Siku kama ya leo miaka 1261 iliyopita, alifariki dunia, Sinan Nukhai al Kufi, aliyekuwa akiitwa kwa lakabu ya Abu Abdillah, mmoja wa wasomi na maulama wakubwa wa elimu ya hadithi mwanzoni mwa kudhihiri dini tukufu ya Uislamu. Sinan, alizaliwa mwaka 95 Hijiria, katika mji wa Bukhara, na ni miongoni mwa wajukuu wa Maliki al Ashtar, kamanda mkubwa na maarufu wa jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as). Abu Abdillah alikuwa mmoja wa mafuqahaa wakubwa wa zama zake na alikuwa kadhi wa mjini wa Kufa nchini Iraq.

Sinan Nukhai al Kufi

Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina. Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China. Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa.

Vita vya China na Japan

Tarehe 25 Julai mwaka 1938 Wapalestina wasio na hatia 62 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina. Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa ni kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina. Wazayuni wamekuwa wakizusha hali ya wasiwasi na vitisho kwa wananchi wa Palestina kwa kushambulia vijiji na maeneo yenye watu wengi katika miji mbalimbali ya Palestina pamoja na kuwauwa shahidi raia wasio na ulinzi, jinai ambazo zinaendelea hadi sasa.

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani. Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadaye alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na fikra za kisiasa. Miongoni wma vitabu vya msomi huyo ni Uislamu na Usoshalisti na Fikra za Kisiasa za Magharibi.

Dakta Hamid Inayat

Na miaka 24 iliyopita katika siku kama hii ya leo, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga, nchi kavu na baharini huko kusini mwa Lebanon. Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.

Mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya ardhi ya Lebanon 1993

 

Tags