Jul 26, 2017 22:50 UTC
  • Alkhamisi Julai 27, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Dhuilqaada 1438 Hijria sawa na 27 Julai, 2017.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo Misri. Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa akidaiwa fadhila na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kuhifadhi maslahi haramu ya Waingereaza hapa Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta na kuitangaza kuwa ya kitaifa, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati. 

Muhammad Reza Pahlavi

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, operesheni kubwa iliyopewa jina la "Mirsad" ilianza huko magharibi mwa Iran kwa lengo la kuwasambaratisha vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin. Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi wa kundi lake hilo wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kwamba wangefika Tehran mara moja na kuuteka mji mkuu. Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka wa Munafiqin huko Magharibi mwa Iran na kuwasambaratisha magaidi hayo wenye uhusiano na nchi za kigeni.

Operesheni ya Mirsad

Katika siku kama ya leo miaka 245 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya ya karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja kati ya nchi zilizo huru za mashariki mwa bara la Ulaya iligawanywa baina ya nchi tatu  kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa kati ya wawakilishi wa Urusi, Austria na Prussia. 

Poland

Miaka 173 iliyopita, John Dalton msomi wa Kingereza alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78. Dalton alibuni na kuvumbua mambo mengi katika uwanja wa fizikia, kemia na sayansi asilia baada ya utafiti mkubwa.  Dalton anahesabiwa kuwa miongoni mwa wasomi mahiri katika historia ya Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa Alexandre Dumas, Fils (mtoto) mwandishi wa vitabu na wa michezo ya kuigiza. Fils alikuwa mwana wa Alexandre Duma, Jenerali wa jeshi na mwandishi wa Kifaransa. Kipindi cha utotoni cha Fils kilikuwa cha mashaka na taabu nyingi, masaibu ambayo ameyataja pia katika athari zake za uandishi.

Alexandre Dumas, Fils

Na miaka 818 iliyopita katika siku kama ya leo, Ibn Munir fakihi na mfasiri wa wa Qur'ami wa Misri alizaliwa huko Alexandria. Alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akaanza kujifunza masomo mbalimbali ya dini kama fikihi, fasihi ya lugha ya Kiarabu na Uluumil Qur’an. Ibn Munir alisoma masomo hayo kwa maustadhi mashuhuri wa zama hizo na kufanikiwa kuwa mtaalamu katika taaluma hizo. Katika kipindi cha uhai wake, Ibn Munir alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ile ya hakimu. Ibn Munir aliaga dunia huko Alexandria nchibni Misri akiwa na umri wa miaka 63 na kuzikwa katika msikiti ambao leo ni mashuhuri kwa jina la Jamiu al-Munir.