Ulimwengu wa Spoti, Julai 31
Hujambo mpenzi msikilizaji wa Radio Tehran na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari katika ulimwengu wa spoti, kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita, karibu.....
Wanakarate wa Iran watwaa medali 5 Mashindano ya Dunia
Wanakarate wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali tano katika Mashindano ya Dunia ya Karate ya mwaka huu 2017 nchini Poland. Medali hizo ni dhahabu moja na fedha nne. Siku ya Jumatano katika ukumbi wa michezo wa GEM jijini Wrocław, magharibi mwa Poland, Muirani Zabiollah Poorsheib alimpeleka mchakamchaka Mjapani Ryutaro Araga katika kitengo cha kumite kwa makarateka wenye kilo 84 na kutwaa dhahabu. Katika safu ya kumite kwa wanamichezo wenye zaidi ya kilo 84 upande wa wanaume, karateka wa Iran Sajjad Ganjzadeh aliibuka wa pili na kutwaa medali ya fedha, baada ya kulemewa na Hideyoshi Kagawa wa Japan. Kadhalika Jumatano hiyo mwanakarate Aliasghar Asiabari aliipa Iran medali ya fedha katika kategoria ya kumite kwa wanakarate wenye kilo 75. Binti wa Kiiran, Hamideh Abbasali aliongeza idadi ya fedha za Iran baada ya kuibuka wa pili katika safu ya wanakarate wa kike wenye kilo 68. Medali nyingine ya fedha ya Iran ilitwaliwa na Amir Mehdizadeh mwenye umri wa miaka 27, baada ya kupelekwa mbio na raia wa Azerbaijan, Firdosi Farzaliyev katika kitengo cha wanakarate wenye kilo 60 mtindo wa kumite. Mashindano hayo ya kimataifa ambayo yalianza Julai 20 na kufunga pazia lake Julai 30 mjini Wroclaw nchini Poland yaliwaleta pamoja wanamichezo zaidi ya 3,200 kutoka nchi 104 duniani.
Muogeleaji wa kike wa Iran aingia katika Daftari la Guiness
Mwanadada bingwa wa mchezo wa kuogelea wa Iran ya Kiislamu ameingia katika Daftari la Kumbukumbu la Guinness. Elham Sadat Asghari mwenye umri wa miaka 36 amefanikiwa kuingia katika daftari hilo la aina yake la dunia, baada ya kuogelea kwa zaidi ya masaa matatu bila kusimama akiwa na pingu mkononi, katika maji ya Ghuba ya Uajemi, katika mji bandari wa Bushehr, yapata kilomita 1,050 kusini mwa mji mkuu Tehran. Siku chache zilizopita mwanadada huyo alitunukiwa cheti ya kuthibitisha kuwa ni miongoni mwa watu wachache waliofanya matukio ya kustaabisha na majina yao kuingia katika daftari hilo linalofahamika kwa Kimbombo kama Guinness Book of World Records.

Muogeleaji huyo mahiri wa Kiirani amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema kuwa: "Nilipitia mengi mazito ili kuvunja rekodi. Uzalendo na kutiwa moyo na marafiki zangu hata hivyo kulinipa motisha na ari ya kutaka kuwa mwanamke wa kwanza wa Iran kutia guu katika Daftari la Kumbukumbu la Guinness."
RAGA: Namibia yatwaa ubingwa wa Africa Gold Cup
Timu ya taifa ya raga ya Namibia imetwaa ubingwa wa Afrika kwa mwaka wa nne mfululizo baada ya kuicharaza Kenya kwa alama 45-7 katika fainali ya Raga ya Afrika (Africa Gold Cup) iliyochezwa Jumamosi katika jiji la Windhoek. Moses Amusala aliifungia Kenya Simbas mguso wa kufutia machozi dakika ya 52, huku Darwin Mukidza akiongeza mkwaju wake. Namibia ambao wamewahi kutwaa taji hilo la kibara mwaka 2002, 2004, 2009, 2014, 2015 na 2016, Namibia, wameibuka kidedea mwaka huu bila kushindwa hata mchuano mmoja.

Timu hiyo awali iliitandika Tunisia 53-7, Senegal 95-0, Zimbabwe 31-26 na Uganda 48-24 kabla ya kuinyoa Kenya na wembe uo huo. Namibia waliwazidi nguvu na kasi vijana wa kocha Jerome Paarwater, ambao pia walifanya makosa mengi yaliyochangia kupoteza mechi yao ya sita mfululizo nchini humo. Kenya, ambao ni mabingwa wa Afrika mwaka 2011 na 2013, walianza kampeni yao kwa sare ya 33-33 dhidi ya mabingwa wa mwaka 2007 Uganda kisha wakaichabanga Tunisia 100-10, Senegal 45-25 na mabingwa wa mwaka 2012 Zimbabwe 41-22 kabla ya kuzidiwa maarifa na Namibia.
2 wafariki dunia katika mkanyagano uwanjani Afrika Kusini
Watu wawili wamethibitishwa kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mkanyagano uliotokea katika uwanja wa FNB nchini Afrika Kusini siku ya Jumamosi. Mkasa huo ulitokea wakati wa mchuano katika ya timu mbili hasimu za Soweto, klabu za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Kuna tetesi kuwa, yumkini mkufunzi wa timu ya taifa ya soka ya Uganda, Milutin Sredojevic almaarufu "Micho" ambaye amevunja mkataba wa kuinoa Uganda Cranes atajiunga na klabu hii ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Shirika la habari la serikali nchini humo SABC limeripoti kuwa, msongamano huo ulitokea katika lango moja la uwanja huo, ambao ulitumiwa katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010. Hata hivyo mchuano huo uliendelea, aghalabu ya mashabiki wasiwe na habari ya mkanyangano na vifo hivyo.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Februari mwaka huu, watu 17 walifariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa nchini Angola baada ya kutokea msongamano mkubwa katika uwanja mmoja wa mpira kaskazini mwa nchi hiyo. Mkasa huo ulitokea katika mji wa Uige katika mechi ya mpira wa miguu kati ya timu mbili za Santa Rita de Cassia na Recreativo do Libolo. Tukio hilo lilitajwa kuwa ni maafa katika historia ya mchezo wa mpira wa miguu nchini Angola.
Mechi za Kimataifa
Klabu ya Manchester City ya Uingereza imeibabadua Real Madrid mabao 4-1 katika msururu wa mechi za timu za Ulaya zinazopigwa kwa ajili ya kupasha misuli moto, huku msimu mpya ukibisha hodi. Mashabiki takriban 93,000 waliisaidia City kushinda mechi yao ya kwanza ya maandalizi ya msimu ujao kupitia mabao yaliyofungwa na Nicolas Otamendi, Raheem Sterling, John Stones na Brahim Diaz huko os Angeles nchini Marekani.

Na tunamalizia kipindi kwa kutupia jicho mchuano ambao uliteka fikra za wengi kati ya mahasimu wawili wakuu wa Uhispania. Bercelona ilisagasaga mahasimu wao Real Madrid kwenye mechi ya Kombe la Michuano ya Kimataifa (ICC) iliyochezwa usiku wa kuamkia Jumapili Miami nchini Marekani. Mechi hiyo iliyoshuhudiwa na mashabiki 66,000 ndiyo ya kwanza kwa mahasimu hao kukutana nje ya Uhispania. Kiungo nyota Lionnel Messi alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kwanza katika dakika ya tatu ya mchezo. Mchezaji Ivan Rakitic aliifungia Barcelona mabao mawili katika dakika saba alizocheza uwanjani. Mabao ya Real Madrid yaliwekwa kimiani na Marco Asensio na Gerard Pigue.
…………………..TAMATI………………