Ijumaa tarehe Mosi Septemba, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 10 Dhulhijja 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Septemba, 2017
Leo tarehe 10 Dhilhaji ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja ya sikukuu kubwa za Kiislamu. Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka huchinja mnyama kutekeleza amri ya Mola kwa ajili ya kujikurubisha kwake na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii adhimu Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu SW alijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumuamuru amchinje mtoto wake kipenzi Ismail (as) naye akatii na kujitayarisha kuitekeleza. Alimlaza chini na kuanza kukata shingo lake lakini kisu kilikataa kuchinja; ndipo Mwenyezi Mungu alipomtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanaye Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawafunza wanadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu SW. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioambatana na uharibifu mkubwa na kuua idadi kubwa ya watu, ulitokea Japan. Zilzala hiyo iliyokuwa na nguvu ya 8.3 kwa kipimo cha Rishta iliua watu zaidi ya laki moja na 40 elfu. Mtetemeko huo uliyakumba hata baadhi ya maeneo ya miji ya Tokyo na Yokohama. Mbali na hasara kubwa zilizosababishwa na mtetemeko huo idadi kubwa ya Wajapan pia walikosa makazi yao na nyumba nyingi ziliteketea kwa moto.
Miaka 48 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomfikisha madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa Mfalme Idris wa Kwanza. Wakati Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi ya kijeshi na kumvua madaraka mfalme huyo sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Hata hivyo katika miaka ya kukaribia kupinduliwa na kuuliwa, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi. Muammar Gaddafi aliondolewa madarakani na kuuawa kufuatia mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011.
Siku kama ya leo miaka 843 iliyopita, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kutundika saa juu yake. Hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda katika masafa ya karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la "Mnara Uliopinda wa Pisa." Hadi kufikia sasa mnara huo umeweza kufanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali.
Siku kama leo miaka 52 iliyopita, yaani tarehe Mosi Septemba mwaka 1961, ulifanyika mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya Isiyofungamana na Upande Wowote NAM huko Belgrade mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 25 duniani. Jumuiya ya NAM iliasisiwa lengo kuu likiwa ni kuziunga mkono nchi za ulimwengu wa tatu mkabala na kambi za Mashariki na Magharibi. Masharti makuu ya kujiunga na jumuiya hiyo, ni kutokuwa mwanachama rasmi katika muungano unaofungamana na madola makubwa ya Mashariki na Magharibi.
Na tarehe 10 Dhulhija miaka miwili iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na azembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia. Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 7 kutoka nchi mbalimbali duniani. Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.