Sura ya Al-Ahzab, aya ya 69-73 (Darsa ya 760)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 69-73 (Darsa ya 760)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 760 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 69 ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا ۚ وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا
Enyi mlio amini! Msiwe kama wale waliomuudhi Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtakasa na waliyo yasema, naye alikuwa mwenye hishima mbele ya Mwenyezi Mungu.
Katika darsa zilizopita na kwenye aya ya 57 ya sura hii ya Ahzab umezungumziwa mwenendo wa wanafiki wa kumuudhi Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa kuzingatia kuwa Mayahudi walikuwa wanaishi katika mji wa Madina na walikuwa na maingiliano na Waislamu, baadhi ya tuhuma na maneno yasiyofaa yaliyokuwa yakisemwa katika zama za Nabii Musa (as) kuhusishwa nayo Mtume huyo wa Allah na ambayo kina Qarun, Firauni na wapinzani wengine wa haki walihusika kuyasambaza yalikuwa yakienea na kufika masikioni mwa Waislamu. Aya hii tuliyosoma inawahutubu waumini kwamba: Jihadharini msije mkawasimulia watu wengine yale mnayoyasikia kwa Mayahudi kuhusu Nabii Musa mkawa mnachangia kueneza uvumi. Sababu ni kwamba Mwenyezi Mungu mwenyewe anashuhudia kuhusu usafi, ukweli na utakasifu wa Mtume wake; hivyo jihadharini kumvunjia heshima mtu ambaye anaheshimika mbele ya Yeye Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya hila zinazotumiwa na maadui ni kudhoofisha na kushusha hadhi za viongozi wa dini kwa njia ya kueneza uvumi, kuzusha tuhuma dhidi yao na hata kuibua shaka juu ya uzima wao wa kimwili na kiakili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa moja ya masharti ya kumwamini kikweli Mwenyezi Mungu ni kuwaamini pia Mitume wake na kwamba hao ni waja wasafi, watakasifu na maasumu; na kujiepusha na kuwazushia tuhuma na uongo wa namna yoyote ile. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mwenyezi Mungu anawalinda waja wake walio safi na watakasifu (hususan Manabii) na tuhuma chafu za maadui na kuwasifu na kuwaenzi. Hivyo na sisi pia tunapaswa kuwa hivyo.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 70 na 71 ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawa.
يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا
Atakutengenezeeni matendo yenu na atakusameheni madhambi yenu. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefuzu kufuzu kukubwa.
Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia ya kuwakataza waumini kueneza maneno yasiyofaa na ya kuudhi wanayoyasikia kwa watu, na kueleza kwamba inapasa mtu ajichunge na kujiepusha kusema jambo lolote ambalo ukweli na usahihi wake haujadhihirika na kuthibitika. Bali waseme neno linaloafikiana na haki na ukweli na si lile linaloweza kutiliwa shaka na kuwa na walakini ndani yake. Ni kusema maneno madhubuti mithili ya ngome imara isiyotetereka na ambayo hayatosababisha kuzuka matatizo ya kifamilia na kijamii. Ni jambo la wazi kwamba ikiwa katika kuzungumza kwao, waumini wote watachunga usuli na vipimo vya uzungumzaji, na kutojiachia waseme mambo kwa kukisia tu na kutoa hukumu juu ya watu kwa kutegemea dhana au kutokana na kuwaangalia kwa jicho baya na kuwa na dhana mbaya tu juu yao, basi jamii itatengenea na kunyooka. Kwa kufanya hivyo wataweza kutatua hatua kwa hatua matatizo ya nyuma na pia kuzuia kutokea matatizo mengine katika mustakbali. Mwenyezi Mungu SW naye pia anawasamehe madhambi yaliyopita watu wanaoacha kusema maneno machafu na yasiyofaa na kuwatengezea mambo yao. Ukweli ni kwamba miongoni mwa mtunda ya taqwa na uchaji Mungu ni kujiweka mbali na kusema maneno yasiyofaa na kushikamana na maneno ya haki na ya sawa. Na hiyo huwa sababu ya waumini kunyookewa mambo yao na kughufiriwa madhambi yao. Katika kuizungumzia taathira ya ulimi na maneno, Imam Sajjad (as) ametoa taabiri ya kuvutia kwa kueleza kwamba, kila siku asubuhi ulimi huvijulia hali viungo vingine vya mwili; na jawabu vinayotoa viungo vyote kuujibu ulimi ni kwamba: Hali zetu ni nzuri, ikiwa wewe utaruhusu (ziwe hivyo)! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba sharti la imani ya kweli ni kuwa na taqwa; na sharti la taqwa ni mtu kusema maneno ya haki na ya sawa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika maneno, uzuri wa utamkaji na upambaji lugha tu hautoshi, bali muhtawa wa maneno yenyewe pia unapasa uwe wenye mashiko na ushahidi madhubuti. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ikiwa mtu atajitahidi kujichunga na kuzingatia taqwa na kumchaMungu ukomo wa uwezo wake, Allah SW atamsamehe pale anapoteleza, na kumuelekeza kwenye njia sahihi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 72 na 73 ambazo zinasema:
إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَن يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ ۖ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا
Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua. Hakika yeye amekuwa dhaalimu mkubwa, mjinga sana.
لِّيُعَذِّبَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ وَيَتُوبَ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗوَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanafiki wanaume, na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na awapokelee toba Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.
Aya hizi ambazo ni aya za mwisho za Suratul-Ahzab zinaashiria maudhui muhimu ya upendeleo aliopewa mwanadamu kulinganisha na viumbe wengine, ambao umetajwa kama 'amana'. Amana ambayo viumbe wengine hawana uwezo wa kuipokea na kufaidika nayo, ni kiumbe aitwaye mwanadamu peke yake ndiye aliyepata rehma za Mwenyezi Mungu za kuweza kufaidika na amana hiyo. Ni wazi kwamba madhumuni ya amana ya Mwenyezi Mungu ni roho, ambayo Yeye Mola amemjaalia kuwa nayo mwanadamu na kumpambanua na viumbe wengine. Roho ambayo ndiyo chanzo cha akili na hisia za utambuzi unaofuatiwa na hiyari na uchaguzi anaojifanyia mwanadamu katika kuhitari njia ya kufuata; na kimsingi ukamilifu wote anaofikia mwanadamu unapatikana kupitia chanzo na chemchemu hiyo. Viumbe wengineo, kuanzia vile visivyo na roho na uhai, mimea pamoja na wanyama hawana uwezo wa kupokea neema hiyo kubwa ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo wamenyimwa. Lakini kutokana na rehma kubwa ya Allah SW juu yake, mwanadamu amejaaliwa kuipata neema hiyo adhimu. Tab’an kama zilivyo neema nyenginezo, neema hiyo pia ni amana ya Mola; na si kwamba yeye mwanadamu ndiye mbunifu na mmiliki wake na akadhani kuwa anaweza kuitumia neema hiyo vyovyote vile atakavyo. Mwenyezi Mungu SW, ambaye ameikabidhi amana hiyo kwa mwanadamu amemtaka kiumbe huyo aitumie katika njia sahihi na kwa ajili ya maslaha na saada yake mwenyewe na jamii yake. Lakini kwa masikitiko ni kwamba wanadamu wengi wametumbukia kwenye lindi la ukafiri au unafiki; na kwa tabia na matendo yao maovu, wamesaliti katika utumiaji wa amana hiyo. Kwa upande wa waumini, ambao wanahisi wao wenyewe kwamba wameitekeleza ahadi ya kuitunza amana hiyo kama walivyotakiwa, huwa mara kadhaa wanateleza na kuitumia amana hiyo kinyume na walivyotakiwa na mmiliki wake Allah SW. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya watu, kutokana na ujinga na kutojua, na baadhi ya wengine kwa sababu ya dhulma zao wameitumia amana ya Allah katika njia isiyo sahihi; na kuna wengine pia waliozembea kuitunza amana hiyo kutokana na taksiri. Ni wazi kwamba wale madhalimu watapata adhabu kwa usaliti walioifanyia amana waliyopewa, na kwa wale waliokosea watapata tena rehma za Mola ikiwa watatubia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwanadamu ni mshika amana ya Mwenyezi Mungu katika ulimwengu. Mola Mwenyezi amempa upendeleo maalumu mwanadamu ambao hakujaaliwa yeyote yule katika viumbe wengine. Upendeleo huo ni hiyo amana ya Allah ambayo inapasa itumiwe kwa namna sahihi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kwa mtazamo wa Uislamu maana ya neno dhulma haihusu kuwatendea dhulma watu wengine tu. Ikiwa mtu atazitumia katika njia isiyo sahihi neema za Mwenyezi Mungu ambazo ni chemchemu za kumjenga na kumfikisha yeye kwenye ukamilifu, atakuwa ameifanyia dhulma kubwa kabisa nafsi yake. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, amana ya Mola ina jukumu na mas-ulia. Ni wazi kwamba yeyote anayefanya usaliti na uhaini katika kutekeleza jukumu hilo la kuitunza amana aliyopewa atafikwa na adhabu ya Mola. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mwanamke na mwanamme wana hali sawa katika kupanda kuelekea kwenye ukamilifu au kuporomoka na kuangukia kwenye hali ya chini kabisa ya udunifu. Na katika mtazamo wa kiutu hakuna tofauti yoyote ile baina ya wawili hao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 760 ya Qur'ani imefikia tamati. Darsa hii pia ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo ya sura yetu hii ya 33 ya Ahzab. InshaaAllah tuwe tumeelimika na kunufaika kwa yote tuliyojifunza katika sura hii pamoja na kupata fadhila za usomaji wake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.