Sep 12, 2017 00:19 UTC
  • Jumanne 12 Septemba 2017

Leo ni Jumanne 21 Dhulhija 1438 Hijria sawa na 12 Septemba 2017.

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita yaani 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa fizikia na kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baba na mama yake walikuwa wasomi mahiri katika fizikia. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mionzi ya nururishi au radioactive.

Irene Joliot- Curie

Miaka 109 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 20 Dhulhija mwaka 1329 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Akhund Mulla Muhammad Kadhim Khorasani, mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu wa Iran. Baada ya kuhitimu elimu yake ya mwanzo mwanazuoni huyo alisoma katika vyuo mashuhuri vya kidini vya Iran na Iraq kupata umashuhuri mkubwa katika elimu za fiqhi na usuli. Akhund Khorasani alifundisha na kulea wanazuoni wakubwa na mashuhuri kama Sayyid Abul Hassan Isfahani, Sayyid Abul Qasim Kashani, Sayyid Muhammad Taqi Khansari, Sayyin Hassan Mudarris, Sheikh Abdul Kariim Hairi, Mirza Hussein Naini na wengine wengi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mashuhuri ni 'Kifayatul Usul' ambacho hadi sasa ni kati ya vitabu vyenye hadhi kubwa katika somo la usulul fiqhi na kinafundishwa kwenye vyuo mbalimbali vya kidini.

yatullah Akhund Mulla Muhammad Kadhim Khorasani

Na katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Selassie. Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia kwa shabaha ya kuyadhibiti. Haile Selassie aliwaajiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya marekebisho ya kidara hatua kwa hatua. Alikomesha utumwa, akafanya marekebisho ya masuala ya kifedha na kuanzisha mfumo wa mahakama nchini Ethiopia. Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1935 yalisitisha mpango wake huo na alibakia nje ya nchi hadi mwaka 1941 aliporejea nchini kwa msaada wa Waingereza na kutwaa tena madaraka. Aliendeleza marekebisho yake ambayo zaidi yalijikita katika mji mkuu Addis Ababa na mambo yasio ya msingi huku sehemu kubwa ya Waethiopia wakikosa suhula za kimsingi za maisha. Selassie alikuwa tegemeza sana kwa nchi za Magharibi. Tarehe 12 Septemba mwaka 1974 Selassie aliondolewa madarakati katika mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo na mwaka mmoja baadaye utawala wa kifalme ulikomeshwa kabisa nchini Ethiopia.

Haile Selassie