Sep 12, 2017 22:05 UTC
  • Jumatano 13 Septemba, 2017

Leo ni Jumatano 22 Dhulhija 1438 Hijria sawa na 13 Septemba 2017.

Siku kama ya leo miaka 1390 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya mfalme wa Iran na Roma. Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani kwa kutekeleza mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo, na hivyo akawa ameweza kupanua wigo wa ushindi wake hadi kufikia Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, hatimaye amani ilifikiwa kufuatia kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe Tano Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyodumu kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili. Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na kumfanya mfalme huyo kukimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Sasania, huku akikataa pendekezo la usuluhishi. Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtukufu Mtume Muhammad (swa) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran kwa kushirikiana na jeshi la taifa walimuengua Khosrow kwenye utawala na kumtia jela kabla ya kuuawa kwake.

Maeneo ya utawala wa Wasasani

Katika siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa na Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). 

Haram na kaburi na sahaba mwema wa Mtume Maytham al Tammar

Siku kama ya leo miaka 957 iliyopita alifariki dunia malenga na arif mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari. Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikwua sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mahabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari

Siku kama ya leo miaka 767 iliyopita, vilianza vita vya Mansuriya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri. Katika vita vya Mansuriya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Sallahuddin Ayubi. Na hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.  

Wakristo wakisalimu amri mbele ya Waislamu

Siku kama ya leo miaka 237 iliyopita, lifti au elevator kwa Kingereza ilivumbuliwa. Mvumbuzi wa lifti hiyo ya kwanza alikuwa raia wa Marekani kwa jina la John Bikbart. Lifti hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza katika mji wa Chicago nchini Marekani. Katika majaribio hayo, watu kadhaa waliingia ndani ya lifti hiyo na kwenda juu na chini. Lifti ya kwanza ya umeme ilitengenezwa mwaka 1889, huku ile ya otomatiki ikitengenezwa mnamo mwaka 1915.

Mfano wa Lifti ya awali

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno. Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika fani ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.

Aquilino Ribeiro

Siku kama hii ya leo miaka 24 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni. 

Makubaliano ya Ghaza-Jericho