Ijumaa tarehe 15 Septemba 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 24 Dhulhija 1438 Hijria sawa na Septemba 15, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1429 kwa mujibu wa nukuu mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake Bibi Fatima (AS), mkwewe Ali bin Abi Twalib (AS) na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (AS) waliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema urongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW).

Miaka 196 iliyopita yaani tarehe 15 Septemba 1821, nchi za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa Uhispania. Baada ya Napoleone Bonaparte mtawala wa Kifaransa kuikalia kwa mabavu Uhispania na kudhoofika serikali ya kijeshi ya Madrid, nchi kadhaa za Latin America zikiwemo Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati. Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1838, nchi wanachama kila moja ilianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya elimu ya tiba, virusi vinavyosababisha ugonjwa hatari wa trakoma au mtoto wa jicho viligunduliwa. Kugunduliwa virusi hivyo kulienda sambamba na njia za kupambana na ugonjwa huo wa mtoto wa jicho, ambapo maelfu ya watu walikuwa wakiwa vipofu katika pembe mbalimbali duniani kutokana na maradhi hayo. Virusi vya trakoma viligunduliwa na matabibu wawili wa Kiingereza.
Na siku kama hii ya leo miaka 18 iliyopita sawa na tarehe 24 mwezi Shahrivar mwaka 1378 Hijria shamsiya, alifariki dunia kwa maradhi ya moyo Dakta Abdulhussein Zarinkub mwanahistoria na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Dakta Abdulhussein alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsiya katika mji wa Burujerd magharibi mwa Iran. Mwaka 1327 Hijria Shamsiya Dakta Zarinkub alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya historia na baadae akaendelea na masomo yake katika taaluma hiyo na kutunikiwa shahada ya udaktari. Mbali na historia msomi huyo wa Kiirani alipenda sana masomo ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na irfani ya Kiislamu. Aidha aliandika vitabu na makala nyingi na moja kati ya vitabu vyake ni kile alichokiita "Alfajiri ya Uislamu."