Sep 17, 2017 02:37 UTC
  • Jumapili, 17 Septemba, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 26 Dhul-Hajj mwaka 1438 Hijiria, sawa na tarehe 17 Septemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 879 iliyopita alizaliwa katika mji wa Wasit nchini Iraq, Abul-Fadhail Amedi mtaalamu wa sheria za Kiislamu na fasihi mkubwa wa Kiislamu. Amedi alisomea elimu za fiqhi, usulu fiqhi, fasihi na hisabati mjini Baghdad. Aidha Abul-Fadhail Amedi mbali na kubobea katika masuala ya sheria za Kiislamu, alikuwa mtaalamu pia katika kusoma mashairi. Amedi alifariki dunia Rabiul-Awwal mwaka 608 Hijiria akiwa na umri wa miaka 49.

Abul-Fadhail Amedi

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, alizaliwa Bernhard Riemann, mwanahisabati maarufu wa nchini Ujerumani. Baba yake Riemann alikuwa askofu masikini ambapo alikuwa akifanya kazi ngumu ili aweze kuandaa vifaa vya masomo vya mtoto wake. Akiwa na umri wa miaka 20 Bernhard Riemann alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Göttingen nchini Ujerumani na kuanza kujifunza elimu ya hisabati ambayo wakati huo ilikuwa mashuhuri sana. Aidha tangu akiwa kijana mdogo alikuwa na kipawa cha hali ya juu katika fani hiyo na ni kwa ajili hiyo ndio maana mara baada ya kujiunga na chuo kikuu moja kwa moja akachagua taaluma ya hesabati, huku akihitimu masomo yake katika ngazi ya PHD akiwa na umri wa miaka 25. Baada ya hapo alianza kufanya uchunguzi na utalii katika taaluma hiyo na kufanikiwa kuwasilisha utafiti wake kwa wahadhiri wa chuo kikuu hapo mwaka 1864. Bernhard Riemann aliaga dunia tarehe 20 Julai mwaka 1866 Miladia akiwa na umri wa miaka 40 kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Bernhard Riemann,

 

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, alifariki dunia Emil Ludwig mwandishi na mwandika wasifu wa Kijerumani. Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin.

Emil Ludwig

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamaji wa Uturuki, Adnan Menderes. Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za Kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki. Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa. Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu. Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62. 

Adnan Menderes

Tarehe 26 Shahrivar miaka 37 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, utawala wa zamani wa Iraq ulifuta kwa upande mmoja makubaliano ya mipaka ya mwaka 1975 yaliyojulikana kwa jina la Mkataba wa Algeria kati yake na Iran. Siku hiyo, Saddam Hussein kiongozi wa zamani wa Iraq aliuchana mkataba huo wa Algeria mbele ya kamera za televisheni akiungwa mkono na madola ya kibeberu. Siku kadhaa baadaye, Saddam Hussein alianzisha uvamizi wa miaka minane dhidi ya ardhi ya Iran.

Mkataba uliovunjwa na Saddam