Jumapili 24 September 2017
Leo ni Jumapili tarehe 3 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria mwafaka na tarehe 24 Septemba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW aliwatumia barua wafalme na watawala mbalimbali duniani na kwa hatua hiyo akawa ameanza rasmi kuwalingania watu Uislamu kimataifa. Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume Muhammad SAW alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa za wakati huo duniani bila ya wasi wasi. Wanahistoria wanasema kuwa, Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine makubwa katika zama hizo ambapo kila mmoja kati ya watawala hao alionesha radimalia yake tofauti. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilionesha wazi kuwa dini ya Kiislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.
Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita yaani tarehe 3 Muharram mwaka 61 Hijria, jeshi la Omar bin Saad liliwasili katika ardhi ya Karbala. Baada ya Hurr bin Yazid kumzingira Imam Hussein AS na maswahaba zake katika ardhi ya Karbala na kuwazuia wasisonge mbele, Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa kibaraka wa Yazid huko Kufa alikabidhi jukumu la ukamanda wa jeshi la Yazid kwa Omar bin Saad.
Siku kama ya leo miaka 610 iliyopita, alizaliwa Ibn Khallouf mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga mkubwa wa Kiislamu. Akiwa kijana mdogo alifanya safari mjini Makkah na baadaye Quds, Palestina huku akisafiri pia mjini Cairo, Misri baada ya kuwa ni kijana. Lengo la safari hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta elimu kiasi kwamba, akiwa na umri wa miaka 26 alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika vyuo vikubwa vya nchini Misri. Mbali na hayo ni kwamba Khallouf alikuwa akisoma pia mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saw) na watu wa familia yake. Hadi leo turathi za msomi huyo zipo katika maktaba za Bairut, Lebanon na Damascus, Syria.
Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita alizaliwa Konstantin Chernenko mmoja wa viongozi wa mwisho wa Urusi ya zamani, kabla ya Mikhail Gorbachev. Chernenko alizaliwa katika familia ya vijijini huko katika mkoa wa Siberia, moja ya mikoa ya Russia ya leo. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi na akiwa na umri wa miaka 18 alikuwa kiongozi wa Shirikisho la Vijana wa Chama cha Ukomonisti cha Urusi ya zamani huku akiteuliwa kuwa mmoja wa viongozi wa chama hicho miaka miwili baadaye. Miaka 20 baadaye aliteuliwa kuwa mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa ofisi ya kisiasa wa chama cha Ukomonisti na baada ya hapo akateuliwa kuwa katibu mkuu wa chama hicho. Konstantin Chernenko alitambuliwa kuwa mtu aliyerithi itikadi za Leonid Brezhnev pamoja na Mikhail Gorbachev. Alifariki dunia tarehe 10 Machi mwaka 1985 akiwa na umri wa miaka 74. Baada ya kufariki kwake dunia Gorbachev aliteuliwa kushika nafasi yake ya uongozi.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw. Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yalidumu kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano ya siku kumi na moja. Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita sawa na tarahe 24 Septamba 1974 nchi ya Guinea Bissau ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Prince Henry mwana wa Mfalme wa Ureno pamoja na wenzake na kuunganishwa na makoloni ya nchi hiyo. Katika karne za 17 na 18 nchi hiyo ilikuwa kituo muhimu cha biashara ya utumwa. Mwanzoni mwa muongo wa 60, harakati za wapigania uhuru zilishadidi na theluthi mbili ya ardhi ya nchi hiyo ikadhibitiwa na wanarakati hao. Mnamo 1974 mkoloni Mreno alilazimika kuutambua uhuru wa Guinea Bissau.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita yaani tarehe Pili Mehr mwaka 1357 Hijria Shamsia, majeshi ya usalama ya utawala wa Baath nchini Iraq yaliizingira nyumba ya Imam Khomeini huko mjini Najaf, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kutokana na utawala wa Baath kuwa na uhusiano mzuri na utawala wa wakati huo wa Shah wa Iran, serikali ya Baghdad ilimtaka Imam Khomeini kutozungumza na vyombo vya habari, kutotoa taarifa wala hotuba zilizobainisha hali ya mambo ilivyokuwa nchini Iran. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema: "Popote nitakapokuwa, sitoacha kutekeleza jukumu langu la kisheria.'' Baada ya muda utawala wa Baath ulimtaka Imam Khomeini aondoke nchini humo.