Sep 25, 2017 02:03 UTC
  • Jumatatu 25 Septemba, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe nne Muharram mwaka 1439 Hijiria, sawa na tarehe 25 Septemba mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) akiwataka kutomsaidia mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba angemuua mtu yeyote ambaye angefanya hivyo. Ibn Ziyad alisoma fatwa iliyokuwa imetolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), na akaamuru kufungwa njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa. bBaada ya hapo aliteremka kwenye mimbari na akaamuru wakazi wa mji huo wapewe fedha na kuwahamasisha kwenda kupigana na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) huko Karbala.

Siku kama ya leo miaka 954 iliyopita alifariki dunia Abul Qasim Muhammad al Baghdadi, mashuhuri kwa jina la Ibn Naafia, ambaye alikuwa mshairi, mwandishi na mwanafasihi mashuhuri wa zama zake. Mashairi yake yalisifiwa sana kutokana na uandishi wake wa kuvutia na diwani kubwa ya mashairi ya Maqaamat inanasibishwa kwa msomi huyo. Katika diwani hiyo Ibn Naafia anaeleza maovu ya kijamii kwa kutumia hekaya, kinaya na vichekesho. Kazi nyingine kubwa ya mwandishi huyo ni al Jiman Fii Tashbihatil Qur'an" kitabu ambacho alikiandika kuthibitisha muujiza wa Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita alizaliwa katika jimbo la Mississippi, Marekani mtaalamu wa fasihi na mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali kwa ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.

William Faulkner

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa huko Baitul Muqaddas.

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita sawa na tarehe 25 Septemba 1997, Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD lilikusudia kumuuwa Khalid Mashal mmoja kati ya shakhsia mashuhuri wa Kipalestina. MOSSAD ikiwatumia wajasusi wake wawili, ilimshambulia na hatimaye kumjeruhi vibaya Khalid Mashal Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, mjini Amman nchini Jordan. Kufeli kwa shambulio hilo na kutiwa mbaroni majasusi hao, kuliwekea alama ya kuuliza uwezo wa shirika hilo la kijasusi la Israel.  Kwa upande mwingine serikali ya Canada ilikasirishwa na kitendo cha majasusi hao wa utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuingia nchini Jordan, huku wakitumia hati za kusafiria za Canada.

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita alifariki dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prof. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupitia makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa nchi za Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya mashariki mwa dunia.

Prof. Edward Said