Ulimwengu wa Spoti, Sep 25
Hujambo mpenzi msikilizaji wa Radio Tehran na karibu tutupie jicho matukio kadhaa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.
Mieleka: Iran yaibuka ya 3 Mashindano ya Kimataifa ya Majeshi
Timu ya taifa ya Iran ya mieleka mtindo wa Greco-Roman imemaliza katika nafasi ya 3 kwenye Duru ya 32 ya Mashindano ya Kimataifa ya Majeshi huko Lithuania. Jumamosi jioni, timu hiyo ya Iran ilitangazwa mshindi wa tatu baada ya kuzoa medali moja ya dhahabu na nne za shaba, mbali na kukusanya pointi 54. Russia iliibuka ya kwanza ikiwa ana alama 59 ikifuatiwa na Ukraine iliyokuwa na pointi 56. Mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama World Military Wrestling Championship yaliyovutia wanamieleka 241 kutoka nchi 22 duniani yalifanyika katika mji wa Klaipeda nchini Lithuania, kati ya Septemba 18 na 25.
Iran yazoa medali chungu nzima Turkemenistan
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo katika nafasi ya pili kufikia sasa kwenye Duru ya 5 ya Mashindano ya Mabingwa wa Michezo ya Ukumbuni na Ustadi yanayoendelea hivi sasa katika mji mkuu wa Turkeministan, Ashgabat. Iran ina medali 77 za dhahabu, 54 za fedha na shaba 65, nyuma ya mwenyeji Turkemenistan yenye jumla ya medali 196. Sohrab Moradi, mnyanyua uzani wa Iran alivunja rekodi siku ya Jumamosi baada ya kunyanyua kilo 413 katika safu ya wanamichezo wenye kilo 94 kwa upande wa wanaume, na kutuzwa medali ya dhahabu.
Siku hiyo hiyo, binti wa Kiirani Zahra Yazdani aliipa Iran dhahabu nyingine katika mieleka mtindo wa Alysh Classic kwa upande wa akina dada wenye kilo zisizozidi 55. Siku ya Jumapili, wanamichezo wa Iran waliibuka kidedea katika mchezo wa snuka katika mashindano hayo ya kieneo, yanayofahamika kama Asian Indoor & Martial Arts Games. Mashindano hayo ya kikanda yalianza Septemba 17 na yanatazamiwa kufunga pazia lake Septemba 27. China yenye jumla ya medali 50 hadi tunaenda mitamboni, inafunga orodha ya tatu bora ya mashindano hayo kwa sasa.
Mnigeria wajiunga na klabu ya Iran
Mchezaji nyota wa kimataifa wa soka raia wa Nigeria Ezekiel Bassey amejiunga na klabu ya Paykan ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 amesaini mkataba wa mmoja na klabu hiyo kwa kima cha pesa ambacho hakikutajwa. Bassey anajiunga na klabu ya Peykan kwa mkopo akitokea klabu ya Enyimba ya Nigeria. Mwanasoka huyo amewahi kuzichezea klabu za Akwa ya Nigeria na Bercelona B ya Uhispania. Anajiunga na raia mwenzake Kenneth Ikechukwu ambaye pia anakipiga hapa nchini.
Riadha: Wakenya watwaa ubingwa Berlin Marathon
Wanariadha nyota wa Kenya Eliud Kipchoge na Gladys Cherono wameibuka kidedea katika mbio za masafa marefu za Berlin Marathon nchini Ujerumani siku ya Jumapili. Kipchoge ambaye alimaliza kwa kutumia masaa mawili, dakika tatu na sekunde 32 nusra avunje rekodi ya dunia, ila hilo likamponyoka kwa sekunde 35. Kipchoge ambaye alishinda mbio hizi mwaka jana na mwaka juzi 2015, mbali na mwezi Mei kubakisha sekunde 25 tu kukimbia muda wa chini ya saa mbili mbio za marathon huko Monza nchini Italia, ametamba huko Berlin na kumuonyesha kivumbi Muethiopia Guye Adole licha ya mvua na kibaridi kikali.
Binafsi ametuma ujumbe wa matumaini kwa vizazi vijavyo, baada ya ushindi huo wa aina yake. Kana kwamba historia ya mwaka 2015 imejikariri tena mwaka huu, mwanadada Gladys Cherono aliibuka wa kwanza katika mbio hizi, kwa kutumia masaa mawili, dakika 20 na sekunde 23. Amesema amefurahishwa na ushindi huo, sambamba na kuvunja rekodi binafsi, huku akiahidi kujinoa ili kufanya vyema zaidi katika siku za usoni. Mwaka 2012, Cherono alikuwa mwanariadha wa kwanza barani Afrika kushinda mbio za Mita 5000 na 10000 wakati wa mashidano ya bara Afrika.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Naibu wake William Ruto wameongoza Wakenya katika mitandao ya kijamii kutuma salamu za pongezi kwa wanaridha hao.
Soka: Afrika Kusini mabingwa
Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Afrika Kusini imetwaa Kombe la Baraza la Mashirikisho ya Soka Kusini mwa Afrika COSAFA baada ya kuizaba Zimbabwe mabao 2-1 katika fainali siku ya Jumapili. Katika kitimutimu hicho kilichopigwa katika Uwanja wa Barbourfields mjini Bulawayo, bao la kwanza la mabinti wa Afrika Kusini wanaojulikana kama Banyana Banyana lilifungwa na Chrestinah Kgatlana dakika chache kabla kwenda mapumzikoni. Zikiwa zimesalia dakika 17 kumalizika mchezo, Zimbabwe walichomoa na kufanya mambo sawa bin sawa, kupitia mchezaji Rutendo Makore. Hata hivyo mabinti wa Banyana Banyana walijipapatua na kucheza mchezo wa kasi zikiwa zimebakia dakika za kuhesabu kwa vidole kipenge cha kumaliza kipindi kipulizwe. Kiungo Leandra Smeda alipachika kimyani bao la ushindi la Afrika Kusini kunako dakika ya 90. Wachezaji Pauline Musungu na Lucy Mukhwana walipoteza penalti zao huku Harambee Starlets ya Kenya ikimaliza mashindano ya hayo COSAFA ya Jumamosi.
Ligi ya Premier
Na tunatamatisha kwa kutupia jicho matokeo ya mechi kadhaa zilizopigwa mwishoni mwa wiki katika Ligi ya Soka ya Uingereza. Manchester City wameendelea na mwendo wao wa kufunga mabao mengi wakiishusha mkiani kabisa Crystal Palace kwa kuichapa mabao 5-0 uwanjani Etihad. Kiungo Leroy Sane aliwazima Palace kwa goli la kwanza la mchezo huo dakika ya 44, kabla ya Raheem Sterling kufunga mabao mawili ya haraka baada ya mapumziko. Sergio Aguero na Fabian Delph pia waliingia kwenye ukurasa wa mabao katika mechi hiyo. Matokeo hayo yanawawafanya City waendelee kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi huku wakiwa na idadi kubwa ya magoli ya kufunga. Kwengineko, Manchester United imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Southampton lakini Jose Mourinho ameilaumu hali ya hewa kwa ushindi huo usiokuwa hafifu katika uwanja wa St. Mary. Huku hayo yakirifiwa, hat-trick ya Alvaro Morata na bao la kiundo mahiri Pedro yaliisaidia Chelsea kuicharaza Stoke City na kuongeza rekodi ya ushindi wao msimu huu. Kwengineko, Everton iliibamiza Bournemouth mabao 2-1 wakati ambapo West Ham walikuwa wanakubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka Tottenham
……………………..TAMATI………………….