Sep 27, 2017 04:12 UTC
  • Jumatano tarehe 27 Septemba, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 6 Muharram 1439 Hijria sawa na Septemba 27, 2017 Miladia.

Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1378 iliyopita mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa wa mjini Madina. "Barua hiyo ilisema: Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga hatapata ushindi." Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba, Imam Hussein alikuwa akijua kuwa, atauawa shahidi yeye na masaba zake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote watauawa na kwamba mtu mwenye malengo mengine bora arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1033 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alifahamika kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za Fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine ya Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihii ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

kaburi la Sayyid Radhi

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki kwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China, Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

Beijing

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.

Tarehe 27 Septemba miaka 21 iliyopita, kundi la Taliban lilivamia na kutwaa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Kundi la Taleban liliasisiwa mnamo mwaka 1994 na likateka hatua kwa hatua maeneo ya kusini na magharibi mwa Afghanistan kwa himaya ya Marekani, misaada ya kisiasa na kijeshi ya Pakistan pamoja na misaada ya kifedha ya Saudi Arabia. Jeshi la serikali ya Afghanistan lililokuwa likiongozwa na Ahmad Shah Mas'ud liliondoka mjini Kabul siku moja kabla ya Taliban kuuteka mji huo. Baada ya kuingia Kabul, kundi la Taliban lilianza kutekeleza sheria kali na zinazoshabihiana na zile za karne za kati dhidi ya wananchi.

Wapiganaji wa kundi la Taliban

Leo ni tarehe 27 Septemba ambayo inasadifiana na siku ya kimataifa ya 'Utalii Duniani.' Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ikaenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.

 

Tags