Sep 29, 2017 02:40 UTC
  • Ijumaa tarehe 29 Septemba, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 8 Muharram 1439 Hijria, sawa na tarehe 29 Septemba, 2017.

Tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yalimalizika kabisa katika mahema ya mjukuu Wa Mtume (saw) Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kuwa, katika siku ya nane ya mwezi Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena. Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia, Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu aliweza kuvumbua kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.

Enrico Fermi

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin. Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.

Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliaga dunia katika ajali ya ndege. Viongozi hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan Ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, ulifanyika uchaguzi huru wa kwanza nchini Angola. Katika uchaguzi huo chama cha MPLA kilichokuwa kikiongoza nchini humo tangu mwaka 1976 kilipata ushindi na kiongozi wake Jose Edward Dos Santos akachaguliwa tena kuingoza nchi hiyo. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno hapo mwaka 1975. Vita vya ndani nchini humo vilihitimishwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa chama cha upinzani cha UNITA Jonas Savimbi.

Tags