Oct 02, 2017 05:36 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 2

Hujambo mpenzi msikilizaji na hususan ashiki wa spoti na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, ndani na nje ya nchi. Karibu....

Mieleka: Wairani washinda medali Russia

Wanamieleka wa mtindo wa Free Style wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Younes Emami na Kamran Ghasempour wameshinda medali ya dhahabu na shaba kwa usanjari huo katika mashindano ya kimataifa ya Mabingwa wa Mieleka ya Dmitry Korkin 2017 nchini Russia. Emami alitunukiwa medali ya dhahabu siku ya Jumamosi baada ya kumepeleka mchakamchaka Mrusi na kumshinda kwa alama 5-1, katika pambano la wanamieleka wenye kilo 65 lililopigwa katika Ukumbi wa Michezo mjini Yakutsk. Muirani mwingine Ghasempour alitia kibindoni medali ya shaba katika safu ya wanamieleka wenye kilo 85. Mashindano hayo ya kimataifa yaliyowavutia wanamieleka kutoka nchi mbambali kama vile Bulgaria, Finland, Georgia, Iran, Japan, Romania, Korea Kusini na Uturuki yalianza Septemba 30 na kumalizika Oktoba Mosi.

Basketboli: Iran yamaliza ya 4 nchini China

Klabu ya mpira wa kikapu ya Petrochimi Bandar Imam ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya nne katika Mashindano ya Mabingwa wa Basketboli barani Asia mwaka huu 2017 huko nchini China. Siku ya Jumamosi, klabu ya Astana ya Kazakhstan ilipata ushindi hafifu wa vikapu 81-78 dhidi ya Iran, katika mchezo uliopigwa katika Ukumbi wa Michezo wa Chenzhou, kusini mwa China.

Iran wakichuana na Lebanon

Al-Riyadhi ya Lebanon iliizaba Kashgar ya China vikapu 88-59 na kutwaa ubingwa. Mashindano hayo ya kieneo yanayojulikana kama Asia Champions Cup na ambayo huandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani (FIBA), yalianza Septemba 22 na kufunga pazia lake Septemba 30, katika mji wa Chenzhou, kusini mwa China.  

Riadha Kenya: Tergat ashika usukani NOCK

Mwanariadha nyota wa zamani wa mbio za Marathon Paul Tergat, ametangazwa kuwa rais mpya wa Kamati ya Olimpiki nchini Kenya NOCK. Hatua hii imekuja baada ya mvutano wa miezi kadhaa kuhusu wajumbe wa kushiriki katika uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kuwachagua viongozi wapya. Tergat alikwenda katika Uchaguzi huo akiwa mgombea pekee na hivyo akatangazwa kuwa rais mpya bila ya kupata ushinda wowote. Tergat mwenye umri wa miaka 48 amesema atatumia uzoefu wake katika mchezo wa riadha kuboresha usimamizi wa michezo ya Olimpiki nchini humo na kuongoza kwa wazi.

Paul Tergat

 

Kazi kubwa inayomsbiri ni kupambana na madai ya ufisadi yaliyowakabili viongozi waliopita, baada ya michezo ya Olimpiki nchini Brazil mwaka 2016. Mbali na hilo, changamoto ya baadhi ya wanaridha wa Kenya kubainika kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini ni suala lingine ambalo lipo mbele yake. Tergat anachukua nafasi ya Kipchoge Keino, aliyeongoza taasisi hiyo kwa muda wa miaka 20.

Ligi ya Premier

Tugeukie baadhi ya michuano ya Ligi Kuu ya Soka Uingereza almaarufu EPL. Klabu ya Arsenal siku ya Jumapili ilijiongezea katika kapu lake alamu 3 muhimu baada ya kuichachafya Brighton mabao 2-0. Nacho Monreal aliwaweka Arsenal kifua mbele kufuatia mkwaju aliosukuma karibu na eneo la penalti baada ya Brighton kushindwa kuondoa mpira eneo hatari. Arsenal walifunga bao la pili baada ya mapumziko kufuatia counter-attack ambayo ilikamilishwa na Alex Iwobi. Baada ya ushindi huo Arsenal sasa wako pointi moja nyuma ya mahasimu Tottenham ambao pia wako nyuma na viongozi wa ligi Manchester City. Manchester United nao wameendeleza rekodi nzuri msimu huu ya kutofungwa katika mechi 10. Hii ni baada ya Mashetani Wekundu siku ya Jumamosi kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Crystal Palace ambayo imepoteza michezo yote saba ya Premier League msimu huu bila hata kufunga bao. Mabao ya United ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja hadi sasa, yamefungwa na Juan Mata, Marouane Fellaini aliyefunga mara mbili na Romelu Lukaku.

Mchezaji nyota wa Man U, Romelu Lukaku

Mbali na hayo, Frank Lampard amedai Manchester City ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa dhidi ya Chelsea katika mchezo wao Jumamosi wa Ligi Kuu England. Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea, amedai Blues walitawaliwa kila kona katika uwanja wao wa Stanford Bridge shukrani kwa goli la Kevin de Bruyne mchezaji wa zamani wa timu hiyo. Katika michezo mingine, Bournemouth ilitoka sare ya 0-0 na Leicester City wakati Stoke City ikiichapa Southampton mabao 2-1; mabao ya wenyeji yakifungwa na Mame Biram Diouf na Peter Crouch huku bao la Southampton likifungwa na Maya Yoshida. Richarlison alifunga bao la kusawazisha dakika za lala salama Watford ikitoka nyuma na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya West Bromwich Albion ambayo ilipata mabao mawili ndani ya dakika tatu yakifungwa na Salomon Rondon na Jonny Evans, lakini Abdoulaye Doucoure akapunguza. West Ham imefanikiwa kutoka mkiani mwa Premier League baada ya bao pekee la Diafra Sakho kuipa ushindi dhidi ya Swansea. Katika mchezo wa mapema kabisa, Tottenham ilipata ushindi wa mabao 4-0 ugenini dhidi ya Huddersfield huku mabao yao yakifungwa na Kane aliyefunga mara mbili, Davies na Sissoko.

Ancelloti apigwa kalamu

Klabu ya soka ya Bayern Munich imempiga kalamu nyekundu mkufuzi wake Carlo Ancelotti. Kocha huyo ametimuliwa masaa machache baada ya klabu hiyo kulishwa kichapo cha mbwa cha mabao 3-0 ilipovaana na PSG.  Bodi ya Nidhamu ya klabu hiyo imeamua kumfuta kazi Muitaliano huyo ambaye alikuwa amerithi mikoba ya Pepe Guardiola.

Carlo Ancelotti katika mshangao

Ancelotti mwenye umri wa miaka 58, aliisaidia Bayern kushinda taji la Bundesliga, lakini hawakuweza kufika katika hatua ya muondoano ya Klabu Bingwa barani Ulaya pamoja na nusu fainali ya Bundesliga. Naibu meneja Willy Sagnol ataiongoza klabu hiyo kwa muda. Binafsi alikuwa na haya ya kusema baada ya kufutwa kazi.

……………………TAMATI………………….