Ijumaa tarehe 19 Januari, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na 19 Januari 2018.
Miaka 228 iliyopita siku kama ya leo yaani mwaka 1211 Hijiria, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu mkubwa wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.

Miaka 220 iliyopita inayosadifiana na leo, alizaliwa Auguste Comte mwanafalsafa, mwanahisabati wa Kifaransa na mtaalamu wa falsafa umbile au positivism kwa kimombo. Comte alifikia daraja ya uhadhiri katika hisabati akiwa na umri wa miaka 18 tu. Vitabu mashuhuri vya mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni Auguste Comte and positivism na Early Political Writings. Comte aliaga dunia mwaka 1517.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran wenye imani na umoja walifanya maandamano makubwa kupinga mabaki yaliyosalia ya utawala wa kifalme Shah, yaani serikali ya Shapur Bakhtiyar. Wafanya maandamano hao walitaka serikali hiyo ya kifalme itangazwe kuwa si halali, na pia kung'olewa utawala wa Shah na badala yale kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Siku hiyo Imam Khomeini MA akiwa mjini Paris alitoa ujumbe wa maandishi kwa wananchi wa Iran akisema kama tunavyonukuu: "Kwa uwezo wake Mola hivi karibuni nitaungana nanyi ili niweze kuwatumikia na kushirikiana bega kwa bega na matabaka yote ya wananchi kuelekea katika njia ya kujitawala na kuwa huru Iran." Mwisho wa kunukuu.

Katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, Abdul Rauf Mahmoud al-Mabhuh, mmoja wa makamanda waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS aliuawa shahidi huko Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mabhouh aliuawa na makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel walioingia nchini Imarati wakitumia pasipoti bandia. Mabhuh alizaliwa katika familia iliyoshikamana na dini katika kambi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza, Palestina. Shahidi Mahmoud al-Mabhuh ni miongoni mwa waasisi wa Brigedi ya Izzudeen al-Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Baada ya kupita miezi kadhaa, Israel ilitangaza wazi kwamba, ilihusika na jinai ya kumuua Mabhuh.