Jumatatu tarehe 5 Februari, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 18 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na Februari 5, 2018
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Imamu Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi ya Kiislamu; hatua ambayo ilichukuliwa muda mfupi kabla ya ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika amri yake hiyo, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza malengo na mipango ya Mapinduzi ya Kiislamu na akaitaka serikali ya muda ifanye hima kwa ajili ya kufikiwa malengo hayo. Aidha katika amri hiyo, aliainisha jukumu kuu la serikali ya muda ambalo lilikuwa kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mfumo wa kisiasa utakaotawala hapa nchini, kuandaa uchaguzi na kuunda Baraza la Waasisi kwa ajili ya kutunga Katiba.
Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo." Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza."
Katika siku kama ya leo miaka 989 iliyopita, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi aliaga dunia huko Samarra, Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najjashi alikuwa alimu na msomi mkubwa katika karne ya tano Hijria na alibobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. Kitabu cha Rijali ni miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyo wa Kiislamu.
Na katika siku kama ya leo miaka 1111 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Athari mashuhuri zaidi ya msomi huyo ni kitabu cha al Iqdul -Fariid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi.