Mar 01, 2018 04:33 UTC
  • Alkhamisi tarehe Mosi Machi 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Jamadithani 1439 Hijria sawa na tarehe Mosi Machi 2018.

Tarehe 12 Jamadithani miaka 796 iliyopita aliaga dunia Abul Hassan Ali bin Abdul Samad Hamdani, faqihi, mtaalamu wa lugha na mfasiri wa Qur'ani wa karne ya 7 Hijria. Alizaliwa katika eneo la Sakha nchini Misri na kwa sababu hiyo alipata umashuhuri kwa jina la Sakhawi. Alielekea Sham kwa ajili ya kutafuta elimu zaidi na kuishi mjini Damascus. Sakhawi ameandika vitabu vingi vikiwemo vya al Jawahir, Tuhfatul Faraidh na Sifru al Sa'ada.

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, ufalme wa siku mia moja wa Napoléon Bonaparte ulianza nchini Ufaransa baada ya Bonaparte kutoroka sehemu aliyokuwa amebaidishwa katika kisiwa cha Elba. Tarehe 27 mwezi Februari mwaka huohuo akiwa pamoja na wanajeshi elfu moja Napoleon Bonaparte alifanikiwa kutoroka katika kisiwa cha Elba ambako alikaa akiwa ubaidishoni kwa kipindi cha miezi kumi na kurejea Ufaransa na utawala wa kifalme ukaanza huko Ufaransa.

Napoléon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita yaani tarehe 1 Machi mwaka 1892 Miladia, alizaliwa mjini Tokyo mwandishi na mtaalamu mkubwa wa Japan anayejulikana kwa jina la "Rhunosuke Akutagawa". Mwandishi huyo anahesabika kuwa mmoja wa waasisi wa kanuni mpya za fasihi huko Japan. Akutagawa ameacha athari muhimu na miongoni mwake ni vitabu vya "Binti wa Buibui" na "Tushi Gun." Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1927.

Rhunosuke Akutagawa

Miaka 120 iliyopita siku kama leo, kisiwa cha Puerto Rico kilichoko katika ya Bahari ya Atlantic kaskazini mwa Amerika ya Kusini, kilikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Marekani baada ya kumalizika vita vya kikoloni vya Uhispania na Marekani. Baada ya Marekani kukitwaa kwa nguvu kisiwa hicho ilikifanya ghala kubwa la silaha, kiasi kwamba Marekani iliasisi kambi 13 za kijeshi kisiwani humo. Kisiwa hicho ambacho mara kwa mara hukumbwa na ukosefu wa amani, miongoni mwa nchi zinazozungumza lugha ya Kihispania katika bara la America.

Kisiwa cha Puerto Rico

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita sawa na tarehe 10 Esfand 1357 Hijria Shamsia, Imam Khomeini MA aliwasili katika mji wa kidini wa Qum ulioko kusini mwa Tehran. Mnamo mwaka 1343 Hjria Shamsia, Imam Khomeini alibaidishiwa nje ya Iran na utawala wa Kifalme wa Shah. Hata hivyo mfalme Shah alipinduliwa katika mapambano ya mfululizo ya wananchi Waislamu wa Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA. Baada ya kupinduliwa mfalme Shah, Imam Khomeini MA alielekea katika mji wa Qum katika siku kama ya leo na miezi kadhaa baadaye alilazimika kuhamia mjini Tehran kutokana na wajibu na udharura wa kuweko Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji mkuu na kuongoza harakati za mapinduzi.

 

Tags