Hadithi ya Uongofu (107)
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichotangulia kilijadili maudhui ya pupa na papara katika kufanya mambo.
Tulisema kuwa, pupa au tutuo ni nia ya mtu kutaka kumaliza au kufikia mwisho wa jambo kwa haraka bila ya umakini. Wakati mwingine hali hiyo inafahamika pia kama ni kukosa subira na uvumilivu katika kufanya jambo. Tulieleza kwamba, pupa na papara au tutuo inatajwa katika vitabu vya maadili ya Kiislamu kama ni haraka na kutokuwa na utulivu katika kufanya mambo.
Aidha tulibainisha kwamba, pupa na haraka humfanya mtu aifanye kazi ambayo kimsingi mazingira yake ya kuifanya bado hayajatimia au bado hayajaandaliwa, ambapo natija ya hilo ni sawa na kuchuma tunda ambalo bado halijaiva au kupanda mbegu za zao fulani kabla ya kuiandaa ardhi husika. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 107 ya mfululizo huu, kitazungumzia suala la staha, umakini, utulivu na kutafakari katika mambo, sifa ambayo ni kinyume cha pupa na papara. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Moja ya sifa muhimu kabisa za kimaadili na zenye nafasi ya aina yake katika maisha ya mtu binafsi, familia, jamii na hata katika mahusiano na mdakhala wa kisiasa na kiuchumi wa mtu ni utulivu na staha. Katika Qur'ani neno Taani yaani utulivu na umakini halijatumika kwa sura ya moja kwa moja. Lakini kutokana na kuwa suala la kufanya mambo kwa pupa na papara limekemewa na kukatazwa, inawezekana kufahamu kwamba, utulivu na umakini katika mambo ni sifa njema na inayopendeza.
Mtume saw amenukuuliwa akisema kuwa, kufanya mambo kwa utulivu na kwa kutaamali ni katika sifa za Mwenyezi Mungu na kuharakisha mambo kunatokana na shetani. Hii ina maana kwamba, wakati mtu anapotaka kuzungumza au anapotaka kuuliza, asiharakishe kufanya hivyo. Kadhalika wakati mtu anapotaka kufanya jambo fulani, awali ya yote anapaswa kuchunguza na kupima engo zote na alifanye hilo baada ya kulitwalii na kutaamali natija ya hilo.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib AS ya kwamba amesema: Kama Mwenyezi Mungu angekuwa anataka angeweza kuziumba mbingu na ardhi kufumba na kufumbua. Aidha aya ya 82 ya Surat Yassin inasema: "Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa."

Hata hivyo licha ya hivyo, Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi katika kipindi cha siku sita au kwa maneno mengine katika duru sita ili awape waja wake funzo la utulivu, subira na kutokuwa na haraka na pupa katika kufanya mambo.
Utulivu, subira na umakini katika mambo, huumfanya mtu achukue hadhari na kuwa na hali ya kutaamali na kutafakari katika kuzungumza na kufanya mambo. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Subira na utulivu katika kufanya mambo na kujiweka mbali na pupa na haraka humuepusha muumini na udhaifu na hali ya kulegalega.
Imam Ali AS amenukuliwa katika hadithi nyingine akisema kuwa, kwamba, utulivu ni ishara ya akili na umakini na kutofanya mambo kwa pupa ni dalili ya ukubwa, kuwa na hadhi na busara.
Hii ina maana kwamba, kama mtu hatakuwa na utulivu na umakini katika mambo, kimsingi angali katika ulimwengu wa utoto na hajapevuka kiakili. Inatarajiwa kutoka kwa kila mtu kwamba, ajiweke mbali na matendo na miamala ya kitoto kwa kadiri anavyokuwa na hivyo kuwa mbali na ulimwengu wa kitoto. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndipo inapowezekana kupima kiwango cha akili na ukubwa wa mtu kupitia miamala yake.
Kwa maana kwamba, kadiri mtu anavyokuwa na miamala ya kitoto basi ni ithbati tosha juu ya kiwango kidogo na akili na alichonacho au kutopevuka kiakili. Aidha hadhi na heshima ya mtu au kwa maneno mengine kuchunga mtu heshima yake ni miongoni mwa maadili ya Kiislamu yaliyotiliwa mkazo katika Uislamu na ambayo yana umuhimu wa aina yake. Kulinda staha, hadhi na heshima yake mtu ni kutokubali kujidhalilisha na kufahamu wapi azungumze, nini azungumze na kukataa kushusha hadi yake kwa kufanya mambo ambayo hayastahiki.
Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa, uzuri wa mtu si katika mavazi na umaridadi wake wa kidhahiri bali ni katika utulivu na kutokuwa kwake na pupa katika mambo.
Kwa hakika kuchunga hadhi na shakhsia kunakoambatana na upole na kufanya mambo kwa utulivu ni katika sifa za watu waumini na wa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 63 ya Surat al-Furqan kwamba:
Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
Kwa msingi huo basi, muumini si mwenye kufanya kiburi, kutakabari au kufanya mambo kwa pupa na papara, bali ni mnyenyekevu, mwenye staha na utulivu.
Hata pale anapokutana na wajinga na pengine wakamfanya dhihaka au maudhi, basi yeye huzungumza nao kwa ulaini na si mwenye kuudhika. Sifa ambayo iko mkabala na staha na kuchunga mtu hadhi yake ni kujirahisisha na kujidunisha. Katika hadithi, kujidunisha kunatajwa kuwa ni sifa mbaya na ni ishara ya ujinga.

Kwa hakika kufanya mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana, ni jambo ambalo humfanya mtu aonekane duni na asiye na maana mbele ya watu wengine. Hali hii humfanya mhusika kudunishwa na watu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, muumini hapaswi kufanya jambo ambalo litampotezea hadhi na heshima miongoni mwa watu. Imam Ali bina Abi Twalib AS anaashiria nukta hiyo na kuwataka watu kuifanya hadhi na heshima yao kuwa katika sifa zao kwani mtu anayefanya mamnbo ya kujidunisha na kujishushia hadi humfanya apoteze heshima na hadhi miongoni mwa watu.
Hata hivyo nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni kwamba, baadhi ya wakati miamala ambayo kidhahiri ni ya kitoto, huwa ni vitendo vya hekima na busara. Kama vile mtu mzima kuamua kucheza na watoto na kufanya mambo ya kitoto ili kuwafurahisha watoto na kukidhi haja ya huba na mapenzi wanayohitajia watoto hao.
Tunashuhudia katika historia kwamba, hatua ya Mtume saw na Imam Ali bin Abi Twalib AS ya kucheza na watoto katu haikuwashushia hadhi na daraja yao katika jamii. Hata katika suala la kuzungumza na watu, Uislamu unamtaka mtu azungumze na wengine kwa kadiri ya kiwango cha akili na ufahamu wao. Tukirejea vitabu vya hadithi tunakutana na hadithi mashuhuri kutoka kwa Bwana Mtume saw ambaye anawataka watu wazungumze na wengine kwa kadiri ya akili na ufahamu wao. Anasema: Zungumza (zungumzeni na watu) na watu kwa kadiri ya akili na ufahamu wao.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo siku na wasaa kama wa leo.
Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini…..
Na Salum Bendera