Mar 24, 2018 03:58 UTC
  • Jumamosi, Machi 24, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Rajab mwaka 1439 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 24 Machi 2018 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 923 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu  Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq. Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha 'Maqamaat' ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima. ***

Ibn Hariri

 

Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa hadithi wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77. Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hadithi ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu ustawi wa sayansi ya mwanadamu. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa mujibu wa baadhi ya hadithi hizo za Jules Verne.  ***

Jules Verne

 

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, msikiti mkuu wa mji wa Ganja ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Azerbaijan ulikarabatiwa na kufunguliwa upya baada ya kufungwa kwa miaka 70. Msikiti huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1920 na kufunguliwa tena katika muongo wa 80 katika hafla iliyofanyika sambamba na kuswaliwa Swala ya jamaa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, makumi ya misikiti ilikarabatiwa na kutumiwa na Waislamu kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea Urusi ya zamani na katika jamhuri zake na pia kutokana na matakwa ya Waislamu wote wa Jamhuri ya Azerbaijan. ***

Msikiti Mkuu wa mji wa Ganja

 

Na miaka 136 iliyopita katika siku kama ya leo, Robert Koch daktari na mtafiti wa Kijerumani aligundua vijidudu maradhi vinavyosababisha ugonjwa wa kifua kikuu au Tuberculosis vinavyoitwa tubercle bacillus. Koch alifanya utafiti na kutwalii sana kwa zaidi ya miaka 10 ili kutambua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB na hatimaye akafanikiwa kugundua vimelea maradhi hivyo na kuvipa jina lake Baccilus Koch. Mwaka 1905 Miladia, tabibu huyo wa Kijerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fani ya fiziolojia na tiba.

Siku ya kupambana na maradhi ya Kifua Kikuu