Mar 27, 2018 22:19 UTC
  • Jumatano tarehe 28 Machi, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 10 Rajab 1439 Hijria sawa na 28 Machi 2018.

Siku kama ya leo miaka 1244 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Taqi AS alichukua jukumu la kuuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha AS. Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa masaba wa siku hii, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi al Jawad AS ambaye amesema: "Kumtegemea Mwenyezi Mungu ni ngazi ya kuelekea kwenye ukamilifu. Mwenyezi Mungu humuokoa mtu huyo na kila baya na kumlinda na kila uadui."

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky. Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili. Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli. Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani.

Alexei Maximovich Peshkov

Na katika siku kama leo miaka 79 iliyopita, baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo. Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania.

Jenerali Francisco Franco