Mar 29, 2018 00:02 UTC
  • Alkhamisi 29 Machi, 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Rajab 1439 Hijria sawa na 29 Machi, 2018.

Siku kama hii ya leo miaka 116 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 Miladia, alizaliwa mwandishi wa Kifaransa kwa jina la Marcel Ayme. Katika masomo yake ya awali Ayme alisomea uhandisi hata hivyo kutokana na kupatwa na maradhi aliachana na taaluma hiyo. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo. Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni "Beautiful Image", na "The Green Mare".

Marcel Ayme

Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden. Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo na badala yake akaongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.

Emmanuel Swedenborg

Miaka 342 iliyopita katika siku kama ya leo vita baina Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa Ufalme huo na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland.

Siku kama ya leo miaka 445 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.

Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa

Miaka 868 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa hadithi Ibn Asakir. Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata kusoma katika vituo vya kielimu vya mijini Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimashq."