Ijumaa tarehe 30 Machi 2018
Leo ni Ijumaa tarehe12 Rajab 1439 Hijria sawa na 30 Machi, 2018
Siku kama ya leo miaka 1407 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume SAW na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi. Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka. Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.

Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, Russia iliiuzia Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ina ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja huku likiwa jimbo la 49 la Marekani. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, hususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu. Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, maandamano makubwa kwa jina la "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, tarehe 18 Oktoba mwaka 1975 Miladia, mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza wazi hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuanguka utawala wa kifalme wa Shah, lilifanyika zoezi la kura ya maoni ya nchi nzima kwa ajili ya kuainisha mfumo wa utawala nchini hapa. Kura hiyo ya maoni ya kihistoria iliyopokewa kwa wingi na wananchi wa Iran, ilifanyika kwa siku mbili. Kura hiyo ilimalizika kwa kupigiwa wingi wa kura wa silimia 98.2, utawala wa Mfumo wa Kiislamu.
