Mar 31, 2018 22:13 UTC
  • Jumapili, Aprili 01, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 14 Rajab 1439 Hijria, sawa na tarehe Mosi Aprili 2018, Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita yaani tarehe 14 Rajab mwaka wa pili Hijiria, kulijiri vita baina ya Waislamu na washirikiana wa Makka mwanzoni kabisa mwa kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu. Mapigano hayo ya kwanza ya Waislamu baada ya kusimamisha dola mjini Madina, yaliongozwa na Abdullah bin Jahsh Asadi, huku upande wa pili ukiongozwa na Omar bin al Hadhrami ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa Maquraish. Katika mapigano hayo Omar bin al Hadhrami aliuawa. Mapigano hayo yanajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Sariyyatu Abdullah bin Jahsh.

Jina la Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw)

Siku kama ya leo miaka 440 iliyopita, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey, tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657.

William Harvey

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, alizaliwa mjini Schönhausen, Otto Eduard Leopold Bismarck, mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na kansela wa kwanza katika historia ya Ujerumani. Alianza masomo ya msingi mjini Göttingen na baada ya hapo akaanza kujishughulisha na masuala ya udiplomasia mjini Saint Petersburg, Russia ya leo na Paris, Ufaransa hadi mwaka 1862 ambapo aliteuliwa kuwa waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Prussia. Mwaka 1864 Miladia, Bismarck alikuwa kiongozi wa Prussia katika vita vya Ujerumani, Denmark na Austria. Miaka miwili baadaye na akiwa na cheo hicho hicho akaongoza vita vya Prussia na Austria. Vita hivyo vilipelekea kusambaratisha shirikisho la Ujerumani na hatimaye kujiondoa Austria chini ya ufalme wa Ujerumani. Hata hivyo mwaka 1867, kuliundwa shirikisho la Ujerumani ya Kaskazini ambapo Otto Eduard Leopold Bismarck aliteuliwa kuwa kansela. Baada ya kumalizika vita vya Prussia na Ufaransa sawa na tahere 18 Januari 1871, Bismarck alifanikiwa kuunda ufalme wa Ujerumani kupitia juhudi zake kubwa. Ni baada ya hapo ndipo Bismarck akapewa lakabu ya mfalme mkuu na mfalme wa chuma. Alitawala karibu miaka 20 ambapo baadaye alivuliwa cheo hicho na kufariki dunia tarehe 24 Agosti mwaka 1898 Miladia.

Otto Eduard Leopold Bismarck

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, vikosi vya jeshi la Marekani vilifanya mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan. Mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege elfu 10 za kivita za Marekani zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa siku 83. Hata hivyo Wajapan walipambana ipasavyo katika vita hivyo kwa ajili ya kulinda nchi yao kwa kadiri kwamba meli 36 za kivita za Marekani ziliharibiwa kikamilifu na nyingine 369 kutiwa hasara. Vilevile ndege za kivita 763 za Marekani zilitunguliwa. Wajapan pia walipata hasara kubwa katika vita hivyo kwani wapiganaji laki moja na elfu kumi kati ya wapiganaji wote laki moja na elfu ishirini wa kisiwa cha Okinawa waliuawa au kujeruhiwa.

Kisiwa cha Okinawa nchini Japan

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi, faqihi, mfasiri wa Qur'an Tukufu na hatibu mkubwa wa Iran. Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi alizaliwa mwaka 1309 Hijiria, mjini Qum na katika familia ya elimu na maarifa ya dini. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alijiunga na masomo ya hawza kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Mirza Abul-Qasim Kabir Qumi, Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi, huku akisoma pia elimu ya falsafa na theolojia kwa Ayatullah Mirza Ali Akbar Mudares Yazdi ambapo alifanikiwa kufikia ngazi ya juu ya kielimu. Alikuwa miongoni mwa shakhsia waliochangia katika uhamisho wa Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi kutoka mjini Arak kwenda mjini Qum na hatimaye kuasisiwa hawza ya kielimu mjini hapo. Mbali na kubobea katika utafiti na kujibu shubuha mbalimbali za dini nyingine, alikuwa mjuzi katika masuala ya historia na jografia ya dini mbalimbali ambapo alitoa nadharia katika uwanja huo. Aidha maulama mbalimbali na maraaji walikuwa wakiheshimu nadharia zake hususan katika uga wa fiqhi huku Imamu Khomein (MA) akimpa lakabu ya 'Sheikh al-Twaifa'. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Risaalatu al-Dharar' 'Mantwiqul Hussein' na 'Maqswadul-Hussein.'

Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, vibaraka wa utawala wa Baath uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein walivamia na kuvunjia heshima Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji mtakatifu wa Najaf na ya Imam Hussein (as) huko katika mji mtukufu wa Karbala, sambamba na kuyakandamiza mapambano ya Waislamu wa kusini mwa Iraq. Wananchi wa Iraq walianzisha mapambano ya kuuondoa madarakani utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein baada ya muungano wa vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa kutekeleza oparesheni ya kuwaondoa wanajeshi wa Iraq katika ardhi ya Kuwait. Wakati huo wanajeshi wa Marekani walisitisha oparesheni zao za kijeshi na kuungana na wanajeshi wa Saddam ili kumwaga damu za Wairaqi waliokuwa wakiendesha mapambano huku wakiwa kwenye saumu.

Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) mjini Najaf, Iraq

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, sawa na tarehe 12 Farvardin mwaka 1358 Hijiria Shamsia, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki katika kura muhimu na ya kihistoria ya maoni ya kuamua mfumo uliotakiwa kutawala hapa nchini. Kura hiyo ya maoni ilifanyika kwa muda wa siku mbili. Katika kura hiyo ya maoni asilimia 98.2 ya wananchi Waislamu wa Iran waliunga mkono kuanzishwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini. Kuanzia hapo, kila mwaka ifikapo tarehe 12 mwezi Farvardin, Iran huadhimisha siku hii inayojulikana hapa nchini kwa jina la "Siku ya Jamhuri ya Kiislamu."

Siku ya Jamhuri ya Kiislamu.