Jumatatu, Aprili 9, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 22 Rajab 1439 Hijria sawa na Aprili 9, 2018 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 ilipewa jina la Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia baada ya kutangazwa habari ya mafanikio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika teknolojia ya nyuklia na kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na licha ya vikwazo vya nchi za Magharibi.

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita magaidi wa utawala ghasibu wa Israel walifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji ya umati dhidi ya wakazi wa kijiji cha Dier Yasin ambacho kilikuwa na watu karibu mianne yalifanywa njia ya kuasisi dola la Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina. Mauaji hayo yaliongozwa na makundi matatu ya kigaidi ya Wayahudi ambayo ni Irgun la Menachem Begin, Haganah la David Ben-Gurion na Stern Gang lililokuwa likiongozwa na Isaac Shamir. Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi wake ambao hawakuwa na hatia yoyote. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama.
Tarehe 9 Aprili miaka 26 iliyopita Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade. Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao. Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi.
Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.