Hadithi ya Uongofu (112)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfulizo huu wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu
Kipindi hiki hujadili maudhui mbalimbali za kijamii, kisiasa, kimaadili, kidini na kadhalika na kukunukulieni hadithi na miongozo ya Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu AS. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia uongo ambao sio haramu nao ni uongo wa maslahi. Tulisema kuwa, baadhi ya matendo asili na dhati yake ni mabaya na yasiyofaa. Kwa mfano dhulma na kuwakandamiza watu wengine ni jambo baya katika mazingira yoyote yale. Kwa maana kwamba, mwanadamu haruhusiwi kutenda dhulma kwa namna yoyote ile, hata kama anayemtendea dhulma atakuwa ni adui wa dini ya Mwenyezi Mungu. Lakini kuna baadhi ya matendo mengine kama kusema uongo, ambayo huwa haramu katika mazingira mahususi na maalumu.
Tulieleza kwamba, katika baadhi ya mazingira uongo si tu kwamba, ni jambo linalofaa, bali la kupendeza na hata kuwa ni wajibu na lazima. Tulikunukulieni hadithi ya Mtume Muhammad SAW ambaye alimenukuliwa akisema: Kwa hakika Mwenyezi Mungu anapenda uongo ambao uko katika njia ya urekebishaji na anachukia maneno ya ukweli ambayo hupelekea kutokea ufisadi. Kipindi chetu cha leoa ambacho ni sehemu ya 112 ya mfululizo huo, kitajadili maudhui ya kutoa ushahidi wa uongo. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.
Miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu ambayo yamekemewa mno ni kutoa ushahidi wa uongo au kutoa ushahidi ambao si wa kweli na ambao unapingana bayana na ukweli wa mambo. Ushahidi wa uongo hupelekea kuondoka na kudhoofika uadilifu na jambo hilo linawekwa katika faharasa na orodha moja na madhambi makubwa kama kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
Kama tulivyoashiria hapo awali, kutoa ushahidi wa uongo ni moja kati ya madhambi makubwa. Katika hili mtu anakuwa amefanya dhambi mara mbili. Kwa kutoa ushahidi wa uongo anakuwa kwanza amesema uongo na pili anakuwa ameonyesha haki ni batili au batili ni haki kutokana na ushahidi wake kupindua ukweli. Kutoa ushahidi wa uongo hupelekea kukanyagwa haki za wengine. Kwa maana kwamba, mwenye haki hupoteza haki yake na asiye na haki hupata haki ambayo kimsingi haikuwa ya kwake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana ushahidi wa uongo una adhabu kali kabisa.
Siku moja Bwana Mtume SAW alikuwa akihutubia na katika sehemu moja ya hotuba yake alisema: Enyi watu! Ushahidi wa batili ni mithili ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Kisha akasoma kipande cha mwisho cha aya ya 30 ya Surat al-Haj inayosema:
Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni na usemi wa uwongo.
Aidha Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema katika sehemu nyingine kwamba: Maneno ya mtoaji wa ushahidi wa uongo mbele ya hakimu, hayamaliziki, isipokuwa mhusika anakuwa ameandaliwa nafasi yake katika moto wa Jahanamu. Kwa maneno mengine ni kuwa, kabla ya maneno ya mtu anayetoa ushahidi wa uongo kumalizika, mhusika anakuwa tayari ameandaliwa makazi yake motoni. Shuhuda au mtoa ushahidi ni mtu ambaye anataka kuthibitisha kwamba, wakati jambo fulani linatokea alikuweko na alilishuhudia tukio hilo kwa macho yake. Kwa mfano anayetoa ushahidi wa mauaji ni mtu ambaye wakati tukio la mauaji hayo linatokea alikuweko katika eneo husika na kushuhudia fulani akifanya mauaji hayo.
Kwa hakika mtu anayetoa ushahidi ni yule ambaye kabla ya kutoa ushahidi wake anapaswa kuwa alikuweko wakati wa kutokea tukio husika na anapaswa kubainisha ukweli na namna tukio hilo lilivyotokea kwa umakini na bila ya shaka na kukisia. Kwa maana kwamba, wakati anatoa ushahidi hapaswi kutumia maneno kama nadhani, nafikiri au nahisi ilikuwa hivi au vile. Bali anapaswa kuwa na uhakika wa mia kwa mia na kile anachokitolea ushahidi kwani yeye ndiye anayetegemewa kwa ajili ya kutolewa hukumu ya tukio husika.
Hata hivyo la kusikitisha kwamba, hii leo kuna watu huwa tayari kujitokeza mahakamani na kutoa ushahidi wa kesi fulani ilihali hana taarifa na ufahamu kamili wa jambo lenyewe. Wahusika hawa hawatambui kwamba, katika kutoa ushahidi wa uongo, hakuna tofauti kwamba, mhusika anajua kwamba, anasema uongo au hajui. Kwa maana kwamba, si muhimu mhusika awe anajua au hajui kwamba, anasema uongo katika kutoa kwake ushahidi wa uongo. Kwa maneno mengine mepesi zaidi ni kwamba, endapo huna yakini ya mia kwa mia na jambo fulani, basi hupaswi kusimama na kulitolea ushahidi.
Siku moja Bwana Mtume saw alimjibu mtu aliyeuliza kuhusiana na namna ya kutoa ushahidi kwa kumuuliza: Je unaliona jua? Bwana yule akajibu kwa kusema, ndio. Mtume saw akasema: Kila kitu ambacho kiko wazi kwako kama jua, basi kitolee ushahidi, na kama ni kinyume chake basi acha kukitolea ushahidi kitu hicho.
Hadithi hii kwa hakika inaonyesha umuhimu mkubwa wa suala la kutoa ushahidi na kujiepusha mtu asije akatumbukia katika kutoa ushahidi wa uongo bila ya yeye kujua. Nukta nyingine muhimu tunayojifunza kutokana na hadithi hiyo ya Bwana Mtume saw ni kwamba, kama una shaka japo kidogo na jambo unalotaka kulitolea ushahidi, basi unapaswa kuachana na hatua yako ya kutaka kutoa ushahidi. Imekuja katika hadithi nyingine kwamba, usitoe ushahidi isipokuwa kama jambo husika utakuwa unalifahamu kama kiganja cha mkono wako.
Wakati mtu anapotoa ushahidi wa uongo na hakimu au kadhi baadaye akafahamu kwamba, shahidi wa kesi husika alisema uongo, hukumu ya awali inabatilika. Aidha aliyetoa ushahidi wa uongo anapaswa kuadhibiwa mbele ya kadamnasi ili iwe funzo na somo kwa wengine kutothubutu kutoa ushahidi wa uongo. Aidha Imam Ja'afar Swadiq AS amenukuliwa akizungumzia adhabu dhidi ya mtu aliyetoa ushahidi wa uongo kwa kusema: Anayetoa ushahidi wa uongo anapaswa kupigwa mijeledi kulingana na hakimu atakavyoamua kisha wamzungushe katika viunga vyote vya mji na wawaonyeshe watu wengine ili wamtambue na hivyo kupuuza ushahidi wake. Kisha baada ya kusema maneno hayo, Imam Swadiq AS alisoma aya ya 3 na ya 4 za Surat Nuur zinazosema:
Na wanaowasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu. Isipokuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
Baada ya hapo, Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Sama'ah alimuliza Imam AS: Toba ya watu wanaotoa ushahidi wa uongo inakuwaje?
Katika kujibu swali hilo Imam alisema: "Mtu aliyetoa ushahidi wa uongo anapaswa anapaswa kukiri mbele ya hadhara ya watu katika eneo lile lile alilopigiwa mijeledi kwamba, alitoa ushahidi wa uongo na anajuta kwa hatua hiyo na kwamba, anaomba msamaha na toba kwa Mwenyezi Mungu. Wakati huo ndipo itakapofahamika kwamba, ametubu kikweli."
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo, siku na wakati kama wa leo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatu…..