Jumatatu tarehe 16 Aprili 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 29 Rajab 1439 Hijria sawa na Aprili 16, 2018.
Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita ulitokea mlipuko mkubwa ulisababishwa na mtungi wa gesi na kusambaza moto kwenye mahema ya Mahujaji huko Mina kilomita 10 kutoka katika mji wa mtakatifu wa Makka. Mahujaji wasiopungua 343 walifariki dunia na wengine 1,290 kujeruhiwa katika tukio hilo. Aidha mahema yasiyopungua elfu sabini yaliteketea kwa moto huo. Hilo linahesabiwa kuwa tukio kubwa la pili la janga la moto kutokea wakati wa msimu wa Hija. Mnamo mwaka 1975, ulitokea moto mkubwa huko Mina nchini Saudi Arabia uliosababisha vifo vya maelfu ya Mahujaji na wengine wengi kujeruhiwa. Kutokana na matukio hayo, Saudi Arabia ililazimika kuweka katika eneo la Mina, mahema yasiyoshika moto ili kuepusha ajali za moto.

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo Wazayuni waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya zamani wa askari wa Uingereza huko Palestina na kuua Wapalestina 90 na kujeruhi wengine wengi. Kwa upande mmoja, maafa hayo yalitokea wakati askari wa Uingereza walipokuwa wakiondoka katika kambi hiyo na kurejea nchini kwao; na kwa upande wa pili, Wazayuni walikuwa wameshadidisha mauaji hayo ya Wapalestina wasio na hatia kwa lengo la kuasisi dola haramu la Israel. Matokeo ya mauaji hayo yaliyofanyika kwa uratibu wa Uingereza, ilikuwa kuuawa idadi kubwa zaidi ya Waislamu wa Palestina na kutangazwa dola bandia la Israel mwezi mmoja baadaye.
Miaka 129 iliyopita, Charles Spencer Chaplin mcheza filamu na msanii mashuhuri wa tasnia ya filamu alizaliwa katika viunga vya mji wa London Uingereza. Alipokuwa mdogo, alianza na michezo ya kuigiza na kupata umashuhuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa ujana wake, Chaplin alielekea nchini Marekani kwa lengo la kutengeneza filamu. Lakini kutokana na kutengeneza filamu ya ukosoaji na yenye kuonyesha mshikamano wake na matabaka ya kimasikini katika jamii ya Marekani, serikali ya nchi hiyo ilitoa amri ya kubaidishwa kwake mnamo mwaka 1952. Chaplin alikumbana na mazingira magumu ya kufanya shughuli zake nchini Marekani na hivyo akahamia nchini Uswisi pamoja na mkewe. Msanii huyo katika tasnia ya filamu alifariki dunia mwaka 1977.
Siku kama ya leo, miaka 1163 iliyopita, alifariki dunia Abdullah bin Muslim Dinuri, maarufu kwa jina la Ibn Qutaybah akiwa na umri wa miaka 63. Ibn Qutayba alizaliwa mjini Kufah, Iraq na kushika hatamu za ukadhi huko mjini Dinuri, magharibi mwa Iran. Alitabahari katika Qur’ani, Hadithi, mashairi na fasihi. Alimu huyo aliandiandika vitabu mbalimbali katika elimu za Kiislamu maarufu zaidi vikiwa ni “Ta’awiilu Mushkili-Qur’ani”, “Tafsiru Ghariibul-Qur’an”, “Uyunul-Akhbaar”, “Maani ash-Shi’ir” na “Gharibul- Hadith.”