Apr 17, 2018 10:03 UTC
  • Aya na Hadithi (22)

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Katika vipindi viwili vilivyopita tulichunguza na kujadili Aya za 38 hadi 41 za Surat al-Haj na Hadithi zinazozifasiri kwa kwina Aya hizo ambapo tulifahamu kwamba wale watu walioruhusiwa kupigana Jihadi na Mwenyezi Mungu kujilazimisha kuwanusuru kutokana na hilo, ni kundi maalumu la waja wake waumini ambao wamepambika kwa sifa ya kuwa na ikhlasi ya hali ya juu

Waja hao wema huwa hawafuatilii jambo jingine kwenye Jihadi isipokuwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza maamrisho na kuepuka makatazo yake. Huwa na kiwango cha juu che elimu ya kina kuhusiana na uadilifu wa Mwenyezi Mungu na hivyo huwa tayari kuvumilia machungu yote katika njia hiyo kwa ajili ya kuwaokoa waja wake na kusimamisha dini yake tukufu duniani. Kupitia Hadithi tulizosoma katika vipindi hivyo ilibainika wazi kwamba mfano bora na wa wazi zaidi wa waja wema hao ni Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw). Madhumuni hayo yanasisitizwa na Aya nyingine za Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani, mfano ukiwa ni Aya za 111 na 112 za Surat al-Tauba ambazo tunazitegea sikio na kuzisikiliza kwa makini hapa. Zinasema: Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu - wanaua na wanauawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'ani. Na ni nani atimizae ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa. Wanaotubia, wanaoabudu, wanaohimidi, wanaokimbilia kheri, wanaorukuu, wanaosujudu, wanaoamrisha mema na wanaokataza maovu, na wanaolinda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na wabashirie Waumini.

 

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, Aya hizi zinasisitiza kwamba wale walioruhusiwa na Mwenyezi Mungu kupigana Jihadi wana sifa maalumu na za hali ya juu ambazo huwawezesha kuwa na uhusiano maalumu na Mwenyezi Mungu Mtukufu na hivyo kumuhimidi na kuwa na nguvu pamoja na uwezo wa kuvumilia masaibu na machungu yanayopatika katika medani ya Jihadi. Waja hao huwa na maarifa ya kina kuhusiana na mambo mema yanayopaswa kuhimizwa na kutekelezwa na yale maovu yanayopaswa kuepukwa. Vilevile huwa na maarifa na elimu ya kutosha kuhusiana na mipaka ya maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu kiasi cha kuwawezesha kuilinda ipaswavyo mipaka hiyo katika uwanja wa vita na Jihadi. Maana hii tuliyoijua kutokana na Aya hizi na zilizotangulia pamoja na nyingine zinazokuja, inasisitizwa na Hadithi Tukufu ambazo tutanufaika na baadhi yazo hivi punde.

*********

Tunaanza na Hadithi iliyonukuliwa na Sheikh Ali bin Ibrahim katika Tafsiri yake kutoka kwa Imam Ali bin Hussein Zeinul Abideen (as) ambapo anasema kuwa Aya mbili hizi ziliteremka kuwahusu Maimamu mahsusi na kisha akaongeza kwa kusema: 'Dalili ya kuwa Aya hizi ziliteremka mahsusi kwa ajili yao (as) ni pale alipowasifu (Mwenyezi Mungu) kwa sifa ambazo hazijuzu kwa watu wengine wewote wasiokuwa wao….Hivyo wanaoamrisha mema – yaani kwa ujumla na bila masharti – ni wale wanaojua mema yote yawe ni madogo, makubwa, ya kina au ya dhahiri, na wanaokataza mabaya ni wale wanajua kwa kina mambo yote mabaya, yawe ni madogo au makubwa. Wale wanaolinda mipaka ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaoilinda mipaka hiyo iwe ni midogo, mikubwa, ya dhahiri au ya kina zaidi na wala hawawi na sifa hii wasiokuwa Maimamu (as).

Na imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi, Tafsiri ya Ali bin Ibrahim, Majmaul Bayaan na vitabu vinginevyo vya kuaminika kutoka kwa Aba Abdilahi as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Ubbad al-Basri – ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wanaowahudumia wafalme aliyejidhihirisha kuwa mmoja wa wanaofanya zuhudi – alikutana na Ali bin al-Hussein (as) akiwa njiani kuelekea Makka na kumwambia: Ewe Ali mwana wa al-Hussein! Je, umeacha kupigana Jihadi na ugumu wake na kuamua kufanya Hija ambayo ina wepesi hali ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo?....... Hapo Ali bin al-Hussein (as) akamwambia: Kamilisha Aya! Akasema: Wanaotubia, wanaoabudu, wanaohimidi, wanaokimbilia kheri, wanaorukuu, wanaosujudu, wanaoamrisha mema na wanaokataza maovu, na wanaolinda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Baada ya kuisoma Aya hiyo Ali bin al-Hussein (as) alimwambia: Tutakapowaona watu walio na sifa hizo, wakati huo kupigana nao Jihadi kutakuwa ni bora kuliko Hija.'

 

Na baada ya maelezo na hoja hizo za Qur'ani kuhusiana na hakika hii, Imam Swadiq (as) alitolea hoja Hadithi ya Mtume kwa kusema: Aya hii (Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo) ilipoteremka, Mtu mmoja alimuuliza Mtume (saw), je, mtu anayebeba upanga na kupigana vita kisha akauwa hali ya kuwa anafuatilia mambo ya haramu kwenye vita hivyo huwa ni Shahidi? Hapo Mwenyezi Mungu alimteremshia Mtume wake Aya inayosema: Wanaotubia, wanaoabudu hadi mwisho wa Aya….. Mtume (saw) aliifasiri Aya hiyo kwa kusema kuwa makusudio ya Mujahideena wanaouawa shahidi na kupata Pepo kutona na Jihadi hiyo ni wale walio na sifa hizo bora za kumcha Mwenyezi Mungu. Alisema Waja wema hao ni wale wanaotubia dhambi zao, wasioabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na jambo jingine lolote na wanaohimidi na kumtukuza Mwenyezi Mungu katika kila hali ya shida na faraja. Ni wale wanaokimbilia kheri wakikusudiwa hapa wale wanaofunga saumu, kurukuu na kusujudu ambao husimamisha na kuzilinda Swala tano katika muundo wake mzima wa rukuu, sijda na katika kunyenyekea kwenye Swala hizo na kuzisimamisha kwa wakati wake. Ni wale wanaoamrisha mema na kukataza maovu. Alimaliza kwa kusema kuwa yeyote yule anayeuliwa hali ya kuwa ametimiza masharti haya anapasa kubashiriwa mema ya kuuawa shahidi na kupata Pepo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu hajawaamuru watu kupigana Jihadi ila wale waliotimiza masharti haya: Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila tu kwa kuwa wanasema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu!

***********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Aya na Hadithi kwa juma hili. Kipindi hiki kimekujieni kama kawaida kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags