Apr 20, 2018 01:38 UTC
  • Ijumaa tarehe 20 Aprili 2018

Leo ni ijumaa tarehe 3 Shaaban 1439 Hijria sawa na tarehe 20 Aprili mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake Imam Hassan (as). Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu.

Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 216 iliyopita Mawahabi wa Hijaz (Saudi Arabia) walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine hususan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) imekuwa ikilengwa na mawahabi. Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi walidumisha mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala  wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. 

Karbala

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, Ustadh Muhammad Taqi Shariati, mfasiri wa Qur'ani na mwanafikra wa Kiislamu wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Alizaliwa mwaka 1286 Hijria Shamsia na baada ya kumaliza masomo yake ya awali alielekea katika mji mtakatifu wa Mashad hapa Iran na kuanza kusoma masomo ya dini kwa juhudi na hima kubwa. Baada ya muda mfupi alijiunga na harakati za Kiislamu za kueneza utamaduni na maarifa ya Kiislamu. Aidha akiwa mjini humo Ustadh Shariati alianzisha taasisi ya kueneza maarifa halisi ya Uislamu sambamba na kuandaa vikao vya elimu na kufundisha darsa za tafsiri ya Qur'ani.

Ustadh Muhammad Taqi Shariati

Miaka 19 iliyopita inayosadifiana na 20 Aprili 1999, kulitokea maafa makubwa ya mashambulizi yaliyofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari. Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo. Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani.

Columbine High School

Na miaka 8 iliyopita katika siku kama ya leo, mlipuko uliotokea kwenye mtambo wa kuchimba mafuta wa Deepwater Horizon na kuzamisha mtambo huo mali ya Shirika la Mafuta la Uingereza (British Petroleum) kulikosababisha kuvuja mafuta katika Ghuba ya Mexico. Wafanyakazi 11 wa mtambo huo waliuawa na mafuta mengi yaliyokuwa yakivuja kutoka katika kisima hicho yalisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kuwahi kutokea katika karne moja ya hivi karibuni huko Marekani.

 

Tags