Hadithi ya Uongofu (113)
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kama mnakumbuka kipindi chetu kilichopita kilijadili maudhui ya kutoa ushahidi wa uongo na kubainisha jinsi kitendo hicho kilivyokatazwa na kukemewa na mafundisho ya Uislamu na hata kuwekwa katika orodha ya madhambi makubwa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 113 ya mfululizo huu kitazungumzia tabia nyingine mbaya ya kimaadili nayo ni ya kusengenya na kuramba kisogo. Jiungeni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Baadhi ya madhambi wapenzi wasikilizaji yana athari kubwa sana katika maisha ya kijamii na ya mtu binafsi na katika kumporomosha mtu kiroho na katika kufikia ukamilifu wa kiutu, kama ambavyo baadhi ya amali njema zina taathira kubwa mno pia katika kumjenga na kumuinua mtu kiroho na kimaanawi. Kusengenya, ni moja ya madhambi ambayo huwa ni utangulizi wa kufanywa madhambi mengine na kuenea maovu katika jamii. Na hilo huthibiti kwa sura hii, kwamba wakati mtu anapotangaza aibu na mabaya ya watu husababisha kuenea maovu na kuyafanya maovu hayo yazoeleke na kutohisika tena kuwa ni kitu kibaya katika jamii. Katika Uislamu kulinda na kuhifadhi roho, mali, heshima za watu na fikra zao ni jambo la lazima. Imekuja katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’afar Swadiq AS kwamba: Heshima ya Muumini ni zaidi ya heshima ya al-Kaaba. Hii ni kutokana na kuwa, heshima ya mtu ni matokeo ya umri wa maisha, hima, idili na juhudi za mtu, hivyo hailaiki na haifai heshima hiyo ambayo mtu kajikusanyia kwa miaka mingi aje mtu na kuiharibu kwa lahadha moja kutokana tu na ujahili wa mtu au malengo maalumu aliyonayo.
Kusengenya ni miongoni mwa madhambi ambayo hucheza shere hadhi na heshima za watu. Imenukuliwa kutoka kwa

Mtume SAW ya kwamba amesema: Katika usiku wa Miraji nilipita katika kaumu moja na kuwaona watu wa eneo hilo wakijikwangua kwa kucha zao. Nikamuuliza Malaika Jibrili: Hawa ni watu gani na kwa nini wanajikwangua namna hii? Jibril akasema: Hawa ni watu ambao kazi yao ilikuwa ni kusengenya watu wengine na kuharibu heshima za watu kwa kuwasema kwa ubaya. Kwa hakika wengi wetu kutokana na kughafilika au kutoshikamana kikamilifu na mafundisho ya Uislamu, tumetumbukia na kunasa katika dhambi ya kusengenya na kuwaramba visogo watu wengine. Tunapaswa kutambua kwamba, kila ambaye anafanya juhudi za kufichua aibu za watu wengine zilizojificha, Mwenyezi Mungu atamuumbua na kumfedhehesha.
Mafundisho matukufu ya diniya Kiislamu yanatoa miongozo yenye faida kubwa kwa ajili ya kuacha dhambi ya usengenyaji. Miongoni mwa miongozo hiyo ni kwamba: Mtu aliyeamua kutafuta tiba ya ugonjwa wa kusengenya anatakiwa azingatie nukta hii kwamba, badala ya kuhesabu aibu na kasoro za watu wengine, jambo bora kwake yeye ni kufikiria zaidi aibu na kasoro zake mwenyewe. Bwana Mtume Muhammad SAW amesema: "Hongera kwa mtu anayeshughulishwa na aibu zake badala ya aibu za watu".
Aidha Imam Sajjad (AS) amesema: "Mtu anayeuzuia ulimi wake usiwafedheheshe na kuwaharibia watu heshima zao, Mwenyezi Mungu atayafumbia macho madhambi yake Siku ya Kiyama".
Njia nyingine inayomsaidia mtu kuacha dhambi ya kusengenya, ni kuwa na hadhari zaidi katika kuchagua marafiki na watu wa kusuhubiana nao na wa kuchanganyika nao. Hii ikiwa na maana kwamba, achague kufanya urafiki na usuhuba na watu wasio na tabia ya kusengenya, na asikae kwenye vikao na mkusanyiko wa watu wenye tabia hiyo, kwa sababu kukaa kwenye vikao vya usengenyaji huathiri roho na moyo wa mtu atake asitake, na kwa kuzingatia kwamba kusikiliza usengenyaji pia ni haramu, inapasa mtu awe makini zaidi katika suala la kuchagua rafiki na hata katika kutembeleana kifamilia.
Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW imeusiwa kwamba, waumini wanatakiwa wakatae kuchanganyika na kukaa na watu wasengenyaji mpaka watu hao waache tabia yao hiyo. Kwa sababu kujiondoa kwenye kikao au mkusanyiko wowote kwa msingi wa kukataa kujumuika na watu wasengenyaji kunaweza kuwa kinga nzuri sana na yenye taathira kubwa ya kujizuia na dhambi ya usengenyaji, na ni aina mojawapo ya mapambano hasi ya kukabiliana na mambo yanayochochea kufanya dhambi hiyo nzito.

Njia nyengine ya kukabiliana na usengenyaji ni kukumbusha na kutanabahisha kwa kutumia ulimi; yaani mara tu mtu anaposikia mtu fulani amesengenywa, achukue hatua papo hapo ya kumkataza msengenyaji kwa kumueleza bayana kuwa 'usisengenye'!
Njia nyingine ambayo ni ya upole ya kumfanya mtu aache kusengenya, na ambayo inategemea uwezo na werevu wa msikiaji ni kwamba, kama mtu hawezi kuondoka katika hadhara hiyo au kumweleza kinagaubaga msengenyaji kwamba aache kusengenya, basi anaweza angalau kwa uchache kutumia ujanja wa kubadilisha maudhui ya mazungumzo ili kuondoa anga ya hali ya usengenyaji.
Njia nyengine ni mtu kujaribu kujizuia kabisa na mazingira ya kusengenya; yaani ikiwa kuna mtu anataka kuzungumziwa habari zake, mtu anayetaka kuanzisha gumzo kuhusu mtu huyo atafakari kwanza kama uzungumziaji huo utaishia kwenye usengenyaji au la. Ikiwa atahisi kuna uwezekano wa kufanya usengenyaji basi aache kabisa kuanzisha mjadala huo, na kwa njia hiyo ataweza kuondoa kikamilifu viashiria vya kufanyika usengenyaji.
Kuomba auni na msaada kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya dua na munajati pia kunamsaidia mtu kuacha madhambi ikiwemo ya kusengenya. Kila wakati tuwe tunamwomba msaada Mwenyezi Mungu atuwafikishe kuepukana na maradhi angamizi ya kiakhlaqi yakiwemo ya kusengenya.

Abudharr al-Ghiffari mmoja wa masahaba watiifu wa Bwana Mtume SAW anasimulia kwamba: Siku moja nilimuuliza mbora huyo wa viumbe, kusengenya nini? Akajibu kwa kusema: Ni kusema maneno kumhusu ndugu yako Mwislamu ambayo hapendi uyaseme. Nikasema: Ewe Mtume wa Allah, je endapo yale ninayoyasema ni mambo ambayo mtu huyo anayo? Akasema: Tambua kwamba, endapo utasema mambo ambayo yeye anayo, utakuwa umemsengenya na kama uliyoyasema ni mambo ambayo hana, basi utahesabiwa kuwa umemzushia na kumtuhumu.
Kwa hakika mara nyingi usengenyaji hufanyika kwa njia ya ulimi. Lakini wigo wa usengenyaji ni mpana zaidi ya hivyo, kwani hata ishara ya mkono na macho pia yumkini ikawa ni sehemu au aina mojawapo ya usengenyaji.
Msengenyaji anaweza kufanya kazi ya kuichunguza batini yake ili kubaini chanzo na udhaifu hasa unaomfanya atende dhambi hiyo ya kusengenya na kufanya jitihada za kuuondoa. Ikiwa sababu ya kusengenya ni kuandamana na kuchanganyika na watu au marafiki wenye mazoea ya kusengenya inapasa ajue kwamba anamghadhibisha Mwenyezi Mungu kwa kufanya amali hiyo chafu na ovu. Na kama husuda na choyo ndiyo sababu inayomfanya awasengenye watu inapasa mtu atambue pia kwamba, kwa kitendo chake cha kusengenya atakuwa amefanya dhambi mbili kwa pamoja, ambazo ni husuda na usengenyaji.
Na hadi hapa ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa leo, tukutane tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu.
Wassalaamu alaykum Warahamtullahi Wabarakaatuh….