May 24, 2018 04:08 UTC
  • Alkhamisi, Mei 24, 2018

Leo ni Alhamisi tarehe nane Ramadhan mwaka 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 24 Mei mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 764 iliyopita, alifariki dunia Najmuddin Ali Dabiran maarufu kwa jina la Katibi ambaye alikuwa mwanafalsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Hakuna maandiko yanayoashiria historia ya kipindi cha awali cha maisha ya msomi huyu lakini maisha yake yanaonesha kuwa Khaja Nasiruddin Tusi alimtaka Katibi kumsaidia katika kituo chake cha elimu ya nujumu huko Maraghe. Najmuddin Ali Dabiran au Katibi kama anavyojulikana zaidi ameandika vitabu kadhaa kama "Jamiud Daqaiq" na "Hikmatul Ain." ***

 

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq. Siku hii inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa, "Siku ya Muqawama na Ushindi". 

Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia. Mwaka 1936 Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea. ***

Na Miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafunzo ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Chama cha Hizbullah kilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa mno katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon toka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.