Jul 06, 2018 22:12 UTC
  • Jumamosi, 7 Julai, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfunguo Mosi Shawwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe 7 Julai 2018.

 

Siku kama ya leo miaka 327 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Mwanazuoni huyo alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin. ***

Sayyid Neematulllah Jazairi

 

Miaka 211 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Russia na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi mojawapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, ulidumu hadi mwaka 1810. ***

Napoleon Bonaparte

 

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru. Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu. Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru. ***

Visiwa vya Solomo

 

Na tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa. Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo. Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi.