Jul 11, 2018 04:06 UTC
  • Jumatano, 11 Julai, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 27 Shawwal 1439 Hijria sawa na Julai 11, 2018.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Waislamu zaidi ya elfu nane wa mji wa Srebrenica mashariki mwa Bosnia Herzegovina waliuawa kwa umati. Mauaji hayo yalifanywa na Waserbia wenye misimamo mikali. Maafa hayo yalikuwa mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Wanamgambo wa Kiserbia wakiungwa mkono na serikali ya Belgrade, waliuvamia mji wa Srebrenica licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulitangaza eneo hilo kuwa la amani mwaka 1993 na kutumwa askari wa umoja huo katika mji huo. Waislamu wa mji wa Srebrenica walijaribu kuondoka katika mji huo, lakini watenda jinai wa Kiserbia waliwauwa wanaume na watoto wao wa kiume na kuwaruhusu wanawake kuondoka katika mji huo. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wanajeshi wa kulinda amani wa Uholanzi waliokuweko katika eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote ya kuwahami Waislamu hao wa Srebrenica.

Mauaji ya Waislamu wa Srebrenica

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita alifariki dunia Habib Samai mwanamuziki na mpiga sahani ya muziki (santuri). Samai alizaliwa mwaka 1280 Hijria shamsiya. Habib Samai alianza kupenda muziki tangu akiwa mtoto kwa kuzingatia kuwa baba yake alikuwa mwanamuziki. Alianza kujifunza muziki wa santuri akiwa kijana. Habib Samai alijiunga na masomo ya muziki kwa muda fulani na kuhitimu mafunzo ya upigaji muziki wa santuri chini ya mwalimu Abul Hassan Saba na baadaye akaanza kufundisha somo la upigaji muziki wa aina hiyo.

Habib Samai

Miaka 97 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Mongolia ilijitangazia uhuru. Mongolia ina historia kongwe mno. Changiz Khan Moghol alianza kuziteka ardhi za nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 13 na kusonga mbele hadi Ulaya ya mashariki. Mongolia iligawanyika katika sehemu mbili yaani Mongolia ya nje na ya ndani baada kusambaratika utawala wa kifalme wa Wamogholi. Mongolia ya ndani iliijumuisha China, na Mongolia ya Nje ikawekwa chini ya udhibiti wa China mwishoni mwa karne ya 17. 

Bendera ya Mongolia

Miaka 461 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Sebastian Cabot mvumbuzi na mwanabaharia wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Tangu awali alikuwa akifanya safari na baba yake aliyekuwa mwanabaharia na kwa msingi huo akafanikiwa kujifunza mambo mengi yanayohusiana na ubaharia.

Sebastian Cabot

Siku kama ya leo miaka 774 iliyopita, mji wa Baitul Muqaddas ulikombolewa na Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Vita vya Msalaba vilianza mwishoni mwa karne ya 11 Miladia na watu wa Ulaya waliwatwisha Waislamu vita hivyo. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba.

Baitul Muqaddas

Na miaka 1098 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alizaliwa malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (saw) na kizazi chake kitoharifu hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani ya mashairi.