Jul 14, 2018 22:39 UTC
  • Jumapili, Julai 15, 2018

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Dhul Qaadah 1439 Hijiri, inayosadifiana na tarehe 15 Julai 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1266 iliyopita na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya zenye itibari, alizaliwa Bibi Fatwimat Maasumah (as), binti mtukufu wa Imam Musa al-Kadhim bin Ja'far (as) ambaye pia ni mmoja wa Ahlul-Bayti wa Mtume Muhammad (saw). Bibi Fatwimat alikuwa hatibu hodari, mwalimu mwenye uwezo mkubwa, huku akiwa ni kiigizo chema cha zuhdi na uchaji-Mungu. Aidha Bibi Fatwimat alifariki dunia mwaka 201 Hijiria wakati alipokuwa safarini kuelekea mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran wakati alipokuwa anaenda kumuona kaka yake yaani Imam Ali Ridha (as) ambapo alipatwa na maradhi na baada ya kukaa kwa muda wa siku 17 mjini Qum kwa ajili ya mapumziko mafupi kutokana na mchoko wa safari. Hii leo kaburi la Bibi Fatwimah hutembelewa na watu mbalimbali duniani mjini Qum kama ambavyo pia ni moja ya maeneo makubwa ya hauza za kielimu na kidini duniani.

Haram ya Bibi Fatwimat Maasumah (as) mjini Qum, Iran

Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 64 Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa visa wa karne ya 19 wa Urusi. Chekhov alikuwa tabibu na katika kujitolea alijenga kituo cha tiba ambacho alikitumia katika shughuli yake hiyo. Baada ya hapo alijiunga na taaluma ya uandishi ambapo alianza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na makala tofauti wakati huo. Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na hivyo kutokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari".

Anton Chekhov

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, mfalme wa Syria aliyewekwa katika nafasi hiyo na Uingereza alifanikiwa kuwa mfalme wa Iraq baada ya kukimbia kutoka Damascus. Julai 15 mwaka 1920, baada ya vikosi vya Ufaransa kukaribia mji wa Damascus, Amir Feisal aliyekuwa ametawalishwa na Uingereza huko nchini Syria aliukimbia mji huo. Syria na Lebanon ni miongoni mwa ardhi zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Othmania ambazo mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia ziliwekwa chini ya udhibiti wa Ufaransa. Tarehe 18 Julai mwaka huo huo, mji wa Damascus ulitekwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya Ufaransa. Amir Feisal ambaye aliongoza Syria kwa miezi mitatu tu akiwa Mfalme, baadaye akatawalishwa na Uingereza kuwa Mfalme wa Iraq.

Faisal, aliyekuwa mfalme wa Syria na kisha Iraq

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea mjini Qum kwa masomo ya juu ya kidini, na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Khomeini MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usulul na falsafa. Akiwa bado kijana, licha ya kuendelea na masomo, lakini alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala wa kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kubaidishwa. Mara baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (MA) mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Muadhamu, lilimchagua Ayatullah Khamenei wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Julai mwaka 1944, jeshi la Marekani lilianza kuishambulia Japan kwa maelfu ya mabomu yaliyodondoshwa na kurushwa na ndege kubwa aina ya B-29 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio hayo ya mabomu ya Marekani yaliendelea hadi Japan iliposalimu amri mbele ya majeshi ya Marekani. Tukio hilo chungu licha ya kusababisha makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan kuuawa kwa halaiki, lilipelekea pia zaidi ya viwanda elfu tatu vikubwa na vidogo kuharibiwa kabisa nchini humo.

Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, Nuri Said Pasha Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq aliuawa baada ya kujiri mapinduzi ya umwagaji damu. AlijIunga na jeshi la utawala wa Othmania akiwa na umri wa miaka 21 na kushiriki katika vita vya utawala wa Othmania na Bulgaria vilivyojiri mwaka 1912. Nuri Said Pasha sambamba na kuwa mwanajeshi, alianzisha harakati za kisiasa na alizingatiwa na Uingereza wakati wa malalamiko ya kisiasa dhidi ya utawala wa Othmania. Hatimaye mwaka 1930 akipata himaya ya Uingereza alichaguliwa kuwa waziri Mkuu wa Iraq.

Nuri Said Pasha Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani alikufa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu katika masomo ya dini. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan na kufungwa jela kwa miaka kadhaa.

Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani

Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa, kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran. Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa kufanyika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Kikundi cha kigaidi kilichojulikana kwa jina la Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi.

Gaidi wa kujitolea muhanga katika Msikiti Mkuu wa Zahedan