Jul 16, 2018 10:11 UTC
  • Jumatatu tarehe 16 Julai 2018

Leo ni Jumatatuu tarehe Pili Dhul Qaada 1439 Hijria sawa na 16 Julai 2018

Siku kama ya leo miaka 3 iliyopita aliaga dunia Sayyid Mutawally Abdul Aal, qari na msomaji mashuhuri wa Qur'ani wa Misri. Abdul Aal alizaliwa mwaka 1947 katika kijiji kimoja cha mkoa wa al Sharqiyyah na kujifunza Qur'ani akiwa bado mdogo. Alifanikiwa kuhifadhi Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka 12. Sayyid Mutawalli Abdul Aal alipata elimu ya kiraa kwa magwiji wa elimu hiyo kama Absul basit Abdul Samad, Mustafa Ismail na hamdi Zamil. Qari huyo mashuhuri alisafiri mara kadhaa nchini Iran na anasema kuhusu Iran kwamba: Sijawahi kuona taifa lolote kama la Iran linaloipenda na kuifia Qur'ani tukufu na kukipa umuhimu mkubwa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. 

Sayyid Mutawally Abdul Aal

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel mkabala wa kukabidhi mabaki ya maiti za askari wawili wa Kizayuni. Mabadilishano hayo ya miili na mateka yalifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani. Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Hizbullah. Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantwari ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.

Samir Qantwar

Miaka 73 iliyopita katika siku kama hii ya leo bomu la kwanza la nyuklia la Marekani liliripuliwa wakati wa majaribio. Marekani ilifanya jaribio hilo la bomu la nyuklia ili kujiandaa kuishambulia Japan kwa kutumia mabomu hayo. Wakati huo Japan ilikuwa ikipigana na madola makubwa na majeshi ya nchi waitifaki, ikiwemo Marekani.

Bomu la nyuklia

Katika siku kama ya leo miaka 128 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

James Parkinson

Na miaka 1128 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokeaji wa hadithi na faqih mashuhuri wa karne ya nne Hijria. Ibn Khuzaima alizaliwa mwaka 223 Hijria na alifanya safari katika pembe mbalimbali duniani wakati wa ujana wake kwa lengo la kujipatia elimu mbalimbali za kidini. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha al Tauhid wa Ithbatl Sifat al Raab.