Jul 28, 2018 02:46 UTC
  • Jumamosi 28 Julai 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1439 Hijria mwafaka na tarehe 28 Julai 2018 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 289 iliyopita, iliyopita harakati ya kwanza ya mapambano ya watumwa weusi wa Marekani ilianza huko kaskazini mwa nchi hiyo. Waanzilishi wa harakati hiyo ambao walikuwa watu 44 walimuua kila mzungu waliyekutana naye katika njia yao kutoka Carolina Kusini kuelekea Florida. Lakini walizingirwa na jeshi la Waingereza na kuuawa kabla ya kuingia Florida na kupata uhuru. Baada ya hapo watumwa weusi waliendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kiraia. Watumwa weusi walikuwa wakitekwa nyara au kununuliwa kutoka Afrika tangu mwanzoni mwa karne ya 17 na kupelekwa Marekani kwa ajili ya kuuzwa na kufanyishwa kazi kwa mabwana zao. ***

Harakati ya watumwa weusi

Katika siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, nchi ya Peru ilijipatia uhuru wake na siku hii hutambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa nchini humo. Peru ilikuwa sehemu ya asili ya watu waliostaarabika wa Inca na tokea karne ya 12 hadi ya 16 ufalme wa watu hao ndio uliotawala kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini. Mwanzoni mwa karne ya 16 wakoloni wa Uhispania waliingia Peru na baada ya mauaji ya kikatili dhidi ya Wahindi wekundu hatimaye ardhi ya Peru ikatawaliwa na wakoloni wa Uhispania. Wahispania waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi hiyo sambamba na kupora mali na raslimali za watu wa Peru hali iliyopelekea kupamba moto mapinduzi ya wapigania uhuru nchini humo. Peru iko kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini, huku ikipakana na nchi za Ecuador, Colombia, Chile, Brazil na Bolivia. ***

Peru

Miaka 140 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Barlin, mwishoni mwa kongamano lililofanyika mjini humo kati ya wajumbe wa nchi za Russia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Austria. Mkutano wa Berlin ulifanyika kwa ombi la kansela wa wakati huo wa Ujerumani Otto Von Bismarck. Kutiwa saini mkataba huo kuliifanya Ujerumani kuwa na satua ya kisiasa na kijeshi na kuandaa uwanja wa kujitanua zaidi nchi hiyo. Kimsingi kutiwa saini mkataba huo wa Berlin kulikuwa moja ya mambo yaliyoandaa uwanja wa kutokea Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.  ***

Mkutano wa Berlin

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, wakati wa kukaribia kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa kifalme wa Austria ulitangaza vita dhidi ya serikali ya Serbia kwa kisingizio cha kuuawa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo huko Serbia. Hata hivyo sababu kuu ya kutolewa tangazo hilo la vita ilikuwa ni upinzani wa wananchi wa Serbia dhidi ya uingiliaji wa Austria katika masuala ya ndani ya nchi yao na pia kufanyika uasi dhidi ya nchi hiyo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, tetemeko kubwa liliukumba mji wa Tangshan mashariki mwa China. Tetemeko hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa7.8 kwa kipimo rishta lilipelekea kuuawa watu wapatao laki sita na malaki kadhaa ya wengine kujeruhiwa sambamba na kuwa wakimbizi. Hata hivyo ripoti rasmi iliyotangazwa na viongozi wa China ilionyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa katika tetemeko hilo ilikuwa laki mbili na 40 elfu. Hilo lilikuwa tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuikumba China katika karne ya 20 na tetemeko kubwa kushuhudiwa tangu tetemeko la mwaka 1556 ambalo lilipelekea kuuawa kwa watu laki nane na elfu 30.

Na miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 6 Mordad 1368 Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki kwenye kura ya maoni ambapo walipiga kura za ndio na kupasisha marekebisho yaliyofanywa katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imam Khomeini (MA) aliagiza kufanyiwa marekebisho katiba ya Iran na kuundwa majlisi kwa ajili ya kutekeleza suala hilo muda mfupi kabla ya kufariki dunia. Miongoni mwa mabadiliko hayo, ni kuondoa sharti la Umarjaa kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa uongozi wa juu nchini, kuogezwa nguvu za rais na kuondoa wadhifa wa Uwaziri Mkuu.

Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ta Iran

 

Tags