Jul 29, 2018 01:21 UTC
  • Jumapili, 29 Julai, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 15 Mfunguo Pili, Dhul-Qaadah 1439 Hijiria, mwafaka na tarehe 29 Julai 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 939 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Faakhir, msomi na mtaalamu mkubwa wa lugha wa Kiislamu. Akiwa kijana alifanya safari tofauti mjini Makkah na Yemen na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo ambapo alitabahari katika elimu ya lugha na hadithi. Aina ya elimu ya Ibn Faakhir ilijengeka juu ya mashairi iliyozingatia vina vya matamshi. Miongoni mwa athari za Ibn Faakhir ni kitabu cha ‘Jawaabul-Masaail.’

Iraq Ibn Faakhir

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa, dikteta na muasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia. Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kuleta aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kukita mizizi nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia.

Benito Mussolini

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, vikosi vya Japan iliyokuwa muitifaki wa Ujerumani wakati wa kujiri Vita Vikuu vya Pili vya Dunia viliwasili katika maeneo ya pwani ya kusini ya India na China kwa ajili ya kuyakalia kwa mabavu maeneo hayo. Kabla ya hapo Japan ilikuwa imelidhibiti na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi za mashariki na kusini mwa China. Katika kipindi cha miaka ya 1941 hadi 1942, Japan ilifanikiwa kuzikalia kwa mabavu ardhi za Thailand, Malaysia, Singapore, Ufilipino, Indonesia na Myanmar ambazo awali zilikuwa chini ya himaya ya Uingereza, Ufaransa na Uholanzi.

Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, uliasisiwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Lengo la kuasisiwa kwa wakala huo lilikuwa ni kusimamia shughuli za vituo vya nyuklia kwa lengo la kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia pamoja na silaha nyingine za maangamizi ya umati. Ofisi ya wakala huo iko mjini Vienna, Austria na maabara yake ya utafiti ipo katika mji huo, ambapo hutoa natija ya chunguzi mbalimbali kuhusiana na matumizi ya nishati ya nyuklia kwa nchi wanachama. Hata hivyo kutokana na kwamba wakala huo umeathiriwa na madola makubwa, umekengeuka malengo yake na kufuata mielekeo ya kisiasa.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, alifariki dunia mwanafikra wa Kijerumani Herbert Marcuse. Marcuse alizaliwa mwaka 1898 na baada ya Wanazi kutwaa madaraka ya nchi hiyo, alielekea Marekani. Herbert Marcuse alikuwa akijitambua kuwa mfuasi wa fikra za Umaxi, ingawa alikuwa akikosolewa na Wamaxi wenyewe. Reason and Revolution na An Essay on Liberation ni baadhi tu ya vitabu mashuhuri vya Herbert Marcuse.

Herbert Marcuse

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Abul Hassan Bani Sadr, Rais aliyeuzuliwa wa Iran aliikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Massoud Rajavi. Siku 37 kabla ya hapo Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha urais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa dikteta Saddam Hussein. Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani. Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevalia nguo za kike.

Abul Hassan Bani Sadr (kushoto)

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Bahlul Gonabadi, alim, mtaalamu wa irfani na mwanamapambano wa Iran. Alizaliwa mwaka 1279 Hijiria Shamsia, katika mji wa Gonabad, kaskazini mashariki mwa Iran. Akiwa na umri wa miaka minane pekee alikuwa amehifadhi Qur’an yote ambapo baada ya kujifunza masomo ya awali ya dini ya Kiislamu, alielekea mjini Mash’had kwa ajili ya masomo ya juu. Ayatullah Muhammad Taqi Bahlul Gonabadi alikuwa shujaa katika kuutetea Uislamu na Waislamu. Wakati Mfalme Reza Shah Pahlavi, dikteta wa zamani wa Iran alipotoa amri ya kuwavua hijabu wanawake wa nchi hii, mwaka 1314 Hijiria Shamsia alitoa hotuba kali ya kupinga amri hiyo ambapo baada ya hapo na kufuatia ukandamizaji mkali wa utawala huo alilazimika kukimbilia Afghanistan na kuendeleza harakati zake za kimapambano. Hata hivyo akiwa nchini humo alikamatwa na kufungwa jela kwa miaka 30.

Ayatullah Muhammad Taqi Bahlul Gonabadi