Aug 05, 2018 12:11 UTC
  • Jumapili , 5 Agosti, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 22 Dhul-Qaadah 1439 Hijiria, sawa na tarehe tano Agosti 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1031 iliyopita, alizaliwa Khoja Nizam al-Mulk, msomi na shakhsia muhimu wa kisiasa na kiutamaduni wa karne ya tano Hijiria mjini Tus, moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran. Nizam al-Mulk alikuwa mmoja wa wasomi ambao walikuwa na taathira kubwa katika mabadiliko ya kisiasa na kiutamaduni katika karne hizo. Katika kipindi cha silsila ya utawala wa Masaljuki, Khoja Nizam al-Mulk aliteuliwa kushika wadhifa wa uwaziri ambapo aliendelea kujishughulisha na masuala ya uongozi kwa kipindi cha miaka 30 na kufanikiwa kuiletea Iran ya wakati huo, maendeleo makubwa hususan katika uga wa utamaduni.

Khoja Nizam al-Mulk

Siku kama ya leo miaka 903 iliyopita, ilimalizika kazi ya uandishi wa tafsiri ya Qur'an Tukufu ya Maj'maul-Bayaan moja ya tafsiri mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu. Tafsiri ya Maj'maul-Bayaan iliandikwa na Sheikh Twabarsi, mmoja wa maulama na wafasiri wakubwa wa Kiislamu. Allamah Twabarsi alikuwa kati ya maulama mashuri wa Iran, ambapo kutokana na uaminifu wake mkubwa aliokuwa nao katika elimu ya fiqhi, hadithi na tafsiri ya Qur'an, alitokea kuwa mashuhuri kwa jina la 'Aminul-Islami, yaani mwaminifu wa Uislamu.' Aidha allamah Twabarsi ameacha athari kadhaa ambapo kila moja inahesabika kuwa na umuhimu mkubwa katika dini ya Kiislamu lakini kubwa zaidi ikiwa ni Tafsir ya Maj'maul-Bayaan fii Tafsirul-Qur'an.

Tafsiri ya Qur'an Tukufu ya Maj'maul-Bayaan

Siki kama ya leo miaka 123 iliyopita alifariki dunia Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.

Friedrich Engels

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Burkina Faso ilipata uhuru. Nchi hiyo ilikoloniwa na Ufaransa kuanzia katikati mwa karne 19. Burkina Faso ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Upper Volta, ilijitangazia mamlaka ya kujiendeshea mambo yake ya ndani mwaka 1958 baada ya kutangazwa mfumo wa jamhuri lakini ilibakia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye katika siku kama hii ya leo Burkina Faso ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Mwaka 1984 jina la Upper Volta lilibadilishwa rasmi na kuwa Burkina Faso.

Burkina Faso

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Marekani, Urusi ya zamani na Uingereza. Baada ya kuanza kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu ulikaribia kutumbukia katika vita vikubwa vya maangamizi kutokana na kuanza majaribio ya nyuklia na utengenezaji wa makombora yanayovuka mabara na yenye vichwa vya silaha za nyuklia. Suala la Cuba na kupelekwa huko makombora ya Urusi liliufanya mgogoro huo ufikie katika kilele. Baada ya kusainiwa mkataba huo anga ya kimataifa ilitulia kidogo na kukaanza mazungumzo kwa ajili ya kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia. Kuanzia Oktoba mwaka 1958 Marekani, Urusi na Uingereza zilitilia maanani suala la kusitisha majaribio ya silaha hizo japokuwa ziliendelea kufanya majaribio hayo. Hatimaye na baada ya mazungumzo mapana, nchi hizo tatu zilifikia makubaliano ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 5 Agosti mwaka 1963.

Utiwaji saini mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Mordad 1367 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini, mwanachuo mashuhuri na mwanamapambano wa Pakistan katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa nchi hiyo. Sayyid A'ref Husseini baada ya kupata elimu ya kidini nchini Pakistan, alifunga safari na kuelekea katika nchi za Iraq na Iran kwa shabaha ya kuongeza maarifa ya kidini. Wakati  wa kutokea  harakati za mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah, Allamah A'ref Husseini alikuwa hapa nchini na kuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, jambo ambalo liliukasirisha utawala wa Shah na kuamua kumfukuza nchini.

Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu  OIC walipasisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu katika mkutano  wa 19 wa mawaziri hao uliofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri. Kwa mnasaba huo siku hiyo imepewa jina la 'Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu.' Tangazo hilo lina utangulizi na vipengee 25. Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu lilipasishwa baada ya nchi za Kiislamu kukosoa Tangazo la Haki za Binadamu lililopasishwa mwaka 1948 katika Umoja wa Mataifa ambalo lilibuniwa kwa misingi ya fikra za kiliberali za nchi za Magharibi na baadhi ya vipengee vyake vinapingana na mafundisho ya Kiislamu. Sifa kuu inayotofautisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu na lile la Umoja wa Mataifa ni kutilia maanani haki za kiroho na kimaanawi za maisha ya mwanadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu  OIC